Kilimo

中国国际广播电台

       

 

China ni nchi yenye idadi kubwa kabisa ya wakulima, na kilimo kinachukua nafasi muhimu sana katika uchumi wa China.

Ingawa eneo la ardhi ya China ni kilomita za mraba milioni 9 na laki 6, lakini ardhi ya mashamba ni kiasi cha kilomita za mraba milioni 1.27, ikiwa ni 7% ya ardhi ya mashamba duniani, ambayo hasa iko katika sehemu ya tambarare ya mashariki na mabonde. Ukulima ni sehemu muhimu sana katika sekta ya kilimo nchini, mazao muhimu ya nafaka ni pamoja na mpunga, ngano, mahindi na maharage, pamoja na mazao ya biashara kama pamba, karanga, mbegu za chakula cha mifugo, miwaa na viazi vitamu.

Maendeleo ya kasi ya kilimo ya China yalianza kutokea baada ya mageuzi ya vijijini mwaka 1978. Katika muda wa zaidi ya miaka 20 iliyopita, mageuzi ya vijijini yakiwa chini ya utaratibu wa umilikaji wa ushirika, yaliondolea mbali vikwazo vya umilikaji wa kijadi na kubuni mikakati mipya ya uchumi wa kimasoko. Mageuzi yalileta manufaa kwa wakulima, na kukuza ufanisi wa nguvu-kazi ya vijijini. Mikakati hiyo ilichangia ongezeko kubwa la kilimo, hususan la uzalishaji wa nafaka, kuboresha hatua kwa hatua muundo wa kilimo na kuleta maendeleo makubwa ya kilimo. Hivi sasa, uzalishaji wa nafaka, pamba, mbegu za chakula cha mifugo, tumbaku, mifugo, mayai, mazao ya baharini na mboga, umechukua nafasi ya kwanza duniani.

Katika miaka ya karibuni, serikali ya China imekuwa ikitoa kipaumbele kwa maendeleo ya kilimo, kuongeza uwekezaji kwa kilimo, kuongeza pato la wakulima na kuleta maendeleo ya uwiano ya miji na vijiji hatua kwa hatua.