Pato na Matumizi ya Wakazi

中国国际广播电台


     
Ikiulinganishwa na miaka zaidi ya 50 iliyopita, kiwango cha maisha ya watu wa China kimeinuka sana, na hata ikilinganishwa na kile cha miaka zaidi ya 20 iliyopita, kimeinuka kwa udhahiri. Pato la watu linaongezeka kwa mfululizo, na mali zao pia zimeongezeka. Hivi sasa watu wa China wanatumia fedha zaidi katika kununua nyumba, magari, kompyuta, vyeti vya hisa na kwenda kutembelea nchi za nje.
Katika kipindi cha miaka zaidi ya 20 baada ya mwaka 1979, uchumi wa China ulipata maendeleo ya kasi, na pato la wakazi pia liliongezeka kwa haraka. Takwimu zilizokusanywa zinaonesha kuwa wastani wa pato la wakazi wa sehemu za vijijini kwa mwaka 2002 ulifikia Yuan 2,476 kutoka Yuan 134 mwaka 1978, na wastani wa ongezeko la pato ulikuwa 7.2% kwa mwaka. Wastani wa pato la wakazi wa mijini ulifikia Yuan 7,703 kutoka Yuan 343, ambalo ni ongezeko la 6.7% kwa mwaka.
Mwaka 2003, maisha ya wakazi wa China yaliendelea kuboreshwa. Wastani wa pato la wakazi wa mijini ulikuwa Yuan 8,472. Na baada ya kuondoa mfumuko wa bei, ongezeko halisi lilikuwa 9%, wastani wa pato la wakazi wa vijijini ulikuwa Yuan 2,622 likiwa ni ongezeko la 4.3%, ambapo fedha za matumizi ya vyakula zilichukua 37.1% ya jumla ya matumizi ya fedha kwa wakazi wa mijini ambalo ni pungufu kwa 0.6%, wakati zile za wakazi wa vijijini zilikuwa 45.6%, ambalo ni pungufu kwa 0.6% pia. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana magari ya binafsi yalifikia milioni 4.89, likiwa ni ongezeko la magari milioni 1.46 kuliko yale ya mwaka uliotangulia.
Hivi sasa hali ya upungufu wa chakula na bidhaa zinazohitajika kwa matumizi ya kila siku, imetoweka kabisa. Mabadiliko ya matumizi ya fedha kwa wakazi yanaonesha kuwa fedha zinazotumika kununua chakula, nguo na mahitaji ya lazima zimepungua, lakini fedha zinazotumika katika kujiendeleza na kununua vitu vinavyoboresha maisha, kama vile nyumba, magari, simu za mikononi, matibabu na utunzaji wa afya, zinaongezeka haraka, na maisha ya wakazi yanaboreshwa hatua kwa hatua.