中国国际广播电台
Majengo ya kasri kwa maneno
mengine ni majengo ya kifalme.
Ni majengo yanayojengwa kwa
ajili ya kuimarisha utawala
wa wafalme, kutukuza heshima
na mamlaka ya wafalme, kukidhi
maisha yao ya anasa kiroho na
kimali. Kwa hiyo majengo hayo
yote yana lengo la kuonesha
ufahari.
Kuanzia
Enzi ya Qin (221-206 K.K.)
nchini China “kasri” lilikuwa
ni makazi ya wafalme na jamaa
wa wafalme, na ni mahali pa
wafalme kushughulikia mambo
ya taifa. Ukubwa wa majengo
ya kasri uliongezeka kutoka
enzi hadi enzi, tofauti yake
na majengo mengine ni paa
la vigae vyenye rangi ya dhahabu,
michoro ya rangi kwenye boriti,
ngazi za marumaru, na majengo
mengine pembeni mwa kasri.
Kasri la Kifalme mjini Beijing
ni kielelezo kizuri cha majengo
hayo.
Ili kutukuza madaraka ya kifalme
na kuonesha kiini cha utawala,
majengo ya kifalme yalikuwa
yakijengwa kwa ulinganifu
kwenye pande mbili za mstari,
majengo yaliyojengwa kwenye
mstari wa katikati ni makubwa
na ya kifahari, na majengo
yaliyokuwa kwenye pande mbili
za mstari wa katikati ni mafupi
na ya kawaida. Kutokana na
maadili ya kijamii nchini
China ikiwa ni pamoja na kuheshimu
mababu, heshima kwa wazee
na kuabudu miungu ya ardhi,
mbele ya kasri kwenye upande
wa kushoto kunajengwa hekalu
la kufanyia tambiko kwa mababu,
na upande wa kulia hujengwa
hekalu la kufanyia tambiko
kwa miungu ya ardhini na nafaka.
Mpangilio huo unaitwa “mababu
upande wa kushoto na miungu
upande wa kulia”. Na majengo
yaliyopo kwenye mstari wa
katikati pia yanagawanyika
katika sehemu mbili, yaani
sehemu ya mbele ni mahali
pa kushughulikia mambo ya
utawala, na sehemu ya nyuma
ni makazi ya wafalme na masuria.
|