中国国际广播电台
Mahekalu ni moja ya aina
ya majengo ya dini ya Buddha
nchini China. Mahekalu nchini
China yalianzia India, mahekalu
hayo ni ishara ya hali ya
ustawi wa dini ya Buddha katika
historia, ni majengo yenye
thamani kubwa kwa ajili ya
uchunguzi na usanii.
Wahenga wa China walizingatia
sana ulinganifu wa majengo
kwenye kando mbili za mstari
wa katikati, hali kadhalika
kwenye ujenzi wa mahekalu
ya dini ya Buddha. Lakini
pia kuna mahekalu yaliyojengwa
kama bustani. Aina hizo mbili
zinayafanya mahekalu nchini
China yawe na taadhima na
uzuri wa kimaumbile.
Mpangilio wa ujenzi wa hekalu
la kale ni kuwa mbele kuna
lango, na baada ya kuingia
kwenye lango hilo upande wa
kushoto na kulia kuna jumba
la kengele na jumba la ngoma,
na nyumba kubwa inayokabili
lango ni ukumbi wa mungu,
ndani ya ukumbi huo kuna sanamu
za walinzi wanne wa peponi,
nyuma ya ukumbi huo na kuendelea
ni ukumbi wa mwasisi wa dini
ya Buddha, Sakyamuni. Ukumbi
huo ni mkubwa na ni muhimu
kabisa kuliko majengo yote
ndani ya hekalu. Mahekalu
yaliyojengwa kabla ya enzi
za Sui (581-618) na Tang (618-907)
kwa kawaida hujengwa pagoda
mbele ya hekalu au katikati
ya ua wa hekalu, na baada
ya enzi za Sui na Tang nafasi
ya jengo la pagoda imechukuliwa
na ukumbi mkubwa, na pagoda
hujengwa katika ua mwingine.
Hekalu la Baimasi
Hekalu hili liko katika mji
wa Luoyang mkoani Henan, lilijengwa
katika Enzi ya Han (206-220
KK.). Hilo ni hekalu la mwanzo
kabisa kati ya mahekalu ya
dini ya Buddha yaliyojengwa
na serikali nchini China.
Ujenzi wake ni wa umbo la
mstatili kwenye eneo la mita
za mraba elfu 40. Ujenzi wa
hekalu hilo ulichangia ustawi
wa dini ya Buddha nchini China
na hata nchi za Asia ya Mashariki
na ya Kusini. Hadi sasa hekalu
hilo linaendelea kuwa mahali
patakatifu kwa waumini wa
dini ya Buddha wa nchi nyingi.
Mahekalu katika Mlima
Wutaishan
Mlima Wutaishan ni sehemu
maarufu ya dini ya Buddha,
kuna majengo 58 ya dini ya
Buddha mlimani, na kati ya
majengo hayo kuna mahekalu
ya Nanchansi na Foguangsi
yaliyojengwa katika Enzi ya
Tang. Hekalu la Nanchansi
ni hekalu lenye miaka mingi
zaidi kati ya mahekalu yaliyojengwa
kwa mbao nchini China. Hekalu
hilo lina sifa zote za mahekalu
ya enzi mbalimbali nchini
China. Kutokana na uhodari
wa ujenzi wake, sanamu, picha
za ukutani na maandishi ya
brashi ya wino, vinasifiwa
kuwa ni “maajabu manne”.
Hekalu la Xuankongsi
Hekalu hili lastahili kutajwa,
kwani ni jengo la ajabu lililojengwa
kwenye genge kali mlimani.
Hekalu hilo liko umbali wa
km. 3.5 kutoka mji mkuu wa
wilaya ya Hunyuan, ni jengo
lililojengwa kwa mbao. Hekalu
hilo lilijengwa katika Enzi
ya Wei Kaskazini (386-534),
na liliwahi kukarabatiwa katika
enzi za Tang, Jin, Ming na
Qing. Hekalu hili linakabiliana
na mlima Hengshan, na hakuna
madaraja ya kupandia, mandhari
yake ni ya ajabu katika mlima
Hengshan.
Kasri la Potala
Madhehebu ya Lama ni moja
ya madhehebu ya dini ya Buddha
nchini China, mahekalu ya
Lama hujengwa kwa ukumbi mkuu
na ukumbi wa kuombea dua.
Mahekalu ya madhehebu ya Lama
hujengwa mbele ya mlima. Kasri
la Potala lililoko mkoani
Tibet ni hekalu la madhehebu
ya Lama, lilijengwa katika
Enzi ya Tang (618-907), na
baada ya enzi nyingi kukarabati
na kupanua kasri hilo limekuwa
na majengo mengi. Kasri hilo
lina eneo la mita za mraba
elfu 20, kuna kumbi kubwa
zaidi ya 20, ndani ya ukumbi
mkubwa wa mbele iliwekwa sanamu
ya shaba ya mwasisi wa dini
ya Buddha, Sakyamuni, iliyopakwa
rangi ya dhahabu kwa kulingana
sawa na mwili wake alipokuwa
na umri wa miaka 12. Kasri
la Potala ni jengo lenye mtindo
halisi wa ujenzi wa Enzi ya
Tang na pia limechukua mitindo
ya India na Nepal.
|