Ujenzi wa Makaburi

中国国际广播电台

      

Ujenzi wa makaburi ni sehemu muhimu katika ujenzi wa China ya kale. Kutokana na imani ya wahenga wa China kuwa roho ya marehemu inadumu milele, mazishi yalikuwa yakitiliwa maanani sana, kwa hiyo watu walikuwa makini sana katika ujenzi wa makaburi. Katika historia ndefu nchini China ujenzi wa makaburi ulipata maendeleo makubwa na makaburi mengi maarufu ya wafalme na malkia yalijengwa. Kutokana na jinsi muda ulivyokuwa ukipita, ujenzi wa makaburi ulichanganywa na sanaa za uchoraji na uchongaji wa sanamu, na kuyafanya makaburi yawe na mkusanyiko wa sanaa za aina nyingi.
Ujenzi wa makaburi nchini China ni mkubwa na wenye majengo mengi. Kwa kawaida ujenzi huo hutumia vizuri sura ya kimaumbile ya ardhi kwenye milima, ingawa pia kulikuwa na makaburi yaliyojengwa katika sehemu za tambarare. Kwa kawaida mpangilio wa majengo ya makaburi huwa na uzio unaozunguka sehemu ya kaburi, na kila upande kuna mlango mmoja, na kwenye kila kona ya uzio kuna jumba la ghorofa, mbele ya kaburi kuna barabara na kwenye pande mbili za barabara kuna sanamu kubwa za mawe za wanyamapori na askari walinzi, ndani ya uzio huo imepandwa misonobari mingi, mazingira hayo yaliwafanya watu kuwa na heshima kubwa kwa marehemu katika hali ya ukimya kabisa.

 

Kaburi la Mfalme Qinshihuang
Kaburi la mfalme Qinshihuang (259K.K.-210K.K.) liko nje ya mji wa Xi’an mkoani Shanxi upande wa kaskazini mwa Mlima Lishan, hilo ni moja ya makaburi maarufu nchini China. Kaburi hilo lilijengwa miaka 2000 iliyopita. Sanamu za askari na farasi zinazosifiwa kuwa ni moja ya “maajabu nane duniani” ni “walinzi wa kaburi” hilo. Sanamu hizo ziliwekwa na UNESCO katika orodha ya urithi wa dunia mwaka 1987. Kamati ya Urithi wa Dunia ilisema, “Sanamu zenye sura mbalimbali za askari, farasi na mikokoteni ya kivita iliyoko pembezoni mwa kaburi la mfalme Qinshihuang ni sanaa adimu aidha iwe katika zama hizi au za kale, zina thamani kubwa za kihistoria.



Sehemu iliyo karibu na mji wa Xi’an lina makaburi mengi ya wafalme, licha ya kaburi la mfalme Qinshihuang, kuna makaburi 11 ya wafalme wa Enzi ya Han Magharibi (206 K.K.-220) na 18 ya wafalme wa Enzi ya Tang (618-907).

Makaburi ya Wafalme wa Enzi ya Ming na Qing
Makaburi ya wafalme wa Enzi ya Ming na Qing ni makaburi ya wafalme yaliyohifadhiwa kikamilifu nchini China.
Makaburi hayo yako katika kitongoji cha Changping nje ya Beijing chini ya mlima Tianshoushan, wafalme 13 walizikwa huko baada ya mji mkuu wa Enzi ya Ming kuhamishwa kwenye mji wa Beijing kutoka mji wa Nanjing. Makaburi hayo yako katika bonde lililozungukwa na milima kwa pande tatu. Kwenye mteremko wa mlima yalipangwa makaburi hayo 13, eneo la makaburi ni kilomita 40 za mraba. Katika sehemu hiyo wamezikwa wafalme 13, malkia 23 na wake wenzao, watoto na mabinti wa wafalme.
Makaburi ya wafalme 13 wa Enzi ya Ming yalijengwa kwa adhama kubwa na penye mandhari nzuri, ni fungu kamili la makaburi ya wafalme nchini China. Kati ya makaburi hayo, kaburi la Changling yaani kaburi la mfalme wa tatu, Zhuli, na kaburi la Ding yaani kaburi la mfalme wa 14 wa enzi ya Ming, Zhuyi, ni makaburi makubwa zaidi. Baada ya kufukuliwa, watu wamegundua kuwa ukumbi wa ardhini bado ni madhubuti ambao ulijengwa kwa mawe wenye nusu duara ya paa kwa mawe, pembeni mwa ukumbi huo kuna mitaro ya maji, na tao la mawe halikutitia, ikionesha ufundi mkubwa wa ujenzi wa ukumbi huo katika China ya kale.

       Sehemu ya mashariki nje ya Beijing kuna eneo la kilomita za mraba 78 za makaburi ya wafalme wa Enzi ya Qing (1616-1991), sehemu ya makaburi ni kilomita za mraba 78, wafalme watano na malkia 14 wa Enzi ya Qing walizikwa huko. Huko makaburi yote yalijengwa kwa makini na ufahari.