中国国际广播电台
China ni nchi kubwa yenye sehemu
tofauti na utamaduni tofauti.
Kutokana na hali hiyo makazi
ya watu pia yanatofautiana.
Katika sehemu wanazokaa watu
wa kabila la Han, makazi ya
watu hujengwa kwa nyumba za
chini zenye nyua za mraba, mfano
wa ujenzi huo ni makazi yaliyopo
mjini Beijing. Nyumba za chini
zenye nyua za mraba mjini Beijing
zimegawanyika kuwa ua wa mbele
na ua wa nyuma. Nyumba iliyopo
katikati ua wa mbele na ua wa
nyuma ni ya heshima kabisa,
ni mahali pa kufanyia sherehe
za familia, na kupokelea wageni
wa heshima. Nyumba zote pembeni
mwa ua wa mbele na ua wa nyuma
zinaelekea katikati ya ua na
zinaunganishwa kwa ujia wenye
paa. Kuishi katika nyumba kama
hizi ni starehe na kwa sababu
ya kuishi pamoja katika nyumba
hizo uhusiano wa jamaa ni wa
karibu sana. Nyumba za aina
hiyo zipo katika sehemu za kaskazini,
na kaskazini mashariki za China.

Nyumba za Ghorofa
za Udongo
Majumba ya ghorofa ya aina
hiyo yanajengwa zaidi katika
sehemu za kusini za China,
umbo la nyumba linakuwa la
duara, mraba au la yai, mithili
ya ngome. Katikati ya jumba
hilo ni kiwanja ambacho kuna
kisima na ghala la nafaka.
Milango ya nyumba ikifungwa
kwa ajili ya kuzuia wezi au
katika siku za vita, watu
wanaoishi ndani ya nyumba
hiyo wanaweza kukaa humo bila
wasiwasi wa kukosa maji wala
chakula kwa miezi kadhaa.
Kwa kawaida nyumba kama hizo
huwa na ghorofa tatu au nne.

Nyumba za ghorofa za udongo
zinajengwa kwa mchanganyiko
wa udongo, kokoto, mchanga
na mbao, katika siku za majira
ya baridi, ndani nyumba kunakuwa
na joto, na katika siku za
majira ya joto ndani ya nyumba
kuwa na baridi, na tena ni
madhubuti hata likitokea tetemeko
la ardhi.
Makazi ya Watu wa
Makabila Madogo Madogo
Makazi ya watu wa makabila
madogo madogo pia yako aina
nyingi. Makazi ya kabila la
Uygur mkoani Xinjiang, kaskazini
magharibi mwa China, yanajengwa
kwa paa lililo bapa, kuta
za udongo na ghorofa moja
au mbili, na kuna ua mbele
ya nyumba; Makazi ya kabila
la Watibet yanajengwa kama
ngome, kuta za mawe kwa nje
na mbao kwa ndani na paa lililo
bapa; Watu wa kabila la Wamongolia
ni wafugaji, wanaishi katika
mahema ambayo ni rahisi kuyahamisha
kufuata malisho ya mifugo;
Watu wa makabila madogo madogo
katika sehemu ya kusini magharibi
mwa China wanaishi katika
nyumba zilizojengwa milimani
karibu na maji, ghorofani
wanaishi watu, na chini inaishi
mifugo au kutunza vitu mbalimbali.
Majumba hayo hujengwa kwa
mianzi na kusimamishwa kwa
nguzo bila kuwa na msingi
ardhini.
Mapango na Makazi
katika Miji ya Kale Kaskazini
mwa China
China ni nchi kubwa yenye
makabila mengi, kwa hiyo makazi
pia ni ya aina nyingi. Makazi
katika sehemu za mwanzo na
katikati ya Mto Huanghe, mengi
zaidi ni ya mapango, makazi
hayo yako katika mikoa ya
Shan’xi, Gansu, Henan na Shanxi.
Wakazi wa sehemu hizo wanachimba
mapango kwenye milima ya udongo
na familia moja huwa na mapango
kadhaa yanayounganishwa kwa
ndani. Kwa ndani mapango hujengwa
kwa matofali. Mapango hayo
hayashiki moto, yanazuia kelele,
na huwa na baridi wakati wa
majira ya joto na joto katika
majira ya baridi, na hayatumii
ardhi ya kilimo.
Nchini China kuna miji ya
kale ambayo mpaka sasa bado
iko vilevile. Ndani ya miji
hiyo kuna makazi mengi ya
kale. Kati ya miji hiyo, mji
wa Pingyao, mkoani Shanxi,
kaskazini mwa China, na mji
wa Lijing, mkoani Yunan kusini
mwa China, imeorodheshwa katika
kumbukumbu za urithi wa dunia
mwaka 1998.

Mji wa Pingyao ni mji kamili
uliobaki tangu Enzi ya Ming
na Qing, ni mfano wa ujenzi
wa miji ya kale katika sehemu
ya kati ya China. Hadi sasa
mji huo bado upo kama ulivyokuwa
zamani. Kuta zake za mji,
barabara, makazi, maduka na
mahekalu bado yapo. Ni sampuli
kwa ajili ya utafiti wa kisiasa,
kiuchumi, kiutamaduni, mambo
ya kijeshi, ujenzi na sanaa
katika histroria ya China.
Mji wa Lijiang ni mji uliokuwepo
toka Enzi ya Song Kusini (1127-1279).
Ujenzi wa mji huo ni mchanganyiko
wa mitindo ya kabila la Wanaxi
na mitindo ya nchi za nje.
Kutokana kutoathiriwa na itikadi
ya kimwinyi iliyotawala sehemu
za ndani za China, barabara
za mjini hazikupangwa kwa
utaratibu, wala hakuna kuta
za mji. Ziwa la Heilong ni
chanzo cha maji, mito midogo
mingi inaanzia kwenye ziwa
hilo na kupeleka maji kwenye
makazi, kwa hiyo ndani ya
mji mito midogo inaonekana
kila mahali, na kwenye kingo
za mito hiyo kuna miti mingi.

|