Majengo katika Enzi ya Song

中国国际广播电台

       Enzi ya Song (960-1279) ilikuwa ni enzi iliyodidimia katika siasa na mambo ya kijeshi, lakini uchumi, viwanda vya kazi za mikono na biashara vilikuwa na maendeleo kwa kiasi fulani, na hasa katika sayansi na teknolojia, hali hiyo iliufanya ufundi wa majengo ufikie kiwango kipya. Majengo katika enzi hiyo yalibadilika kuwa madogo na yenye makini ya mapambo badala ya yale ya majengo makubwa na ya adhama ya Enzi ya Tang.

       Katika miji ya Enzi ya Song yalitokea maduka kwenye barabara, na maduka yalipangwa kwa aina ya bidhaa, na majengo ya shughuli za zimamoto, mawasiliano, uchukuzi, maduka na madaraja, yote yaliendelea kwa hatua kubwa. Sura ya mji mkuu wa Enzi ya Song, Bianliang, (mji wa Kaifeng kwa leo) ilionesha wazi hali ya biashara katika miji ya Enzi ya Song. Katika enzi hiyo, nchini China majengo makubwa makubwa hayakujengwa sana, lakini mapambo na rangi za majengo yalizingatiwa zaidi. Ukumbi katika hekalu la Jinxi mkoani Shanxi ni mfano wa majengo hayo.

Majengo ya matofali yaliendelea zaidi katika Enzi ya Song, majengo hayo yalikuwa ni pagoda ya dini ya Buddha na madaraja. Pagoda katika hekalu la Huilingsi mkoani Zhejiang, pagoda la Fanta katika mji wa Kaifeng mkoani Henan na daraja la Yongtong wilayani Zhaoxian mkoani Hebei yote yanastahili kuwa kama ni mifano ya majengo ya matofali katika Enzi ya Song.

Uchumi wa Enzi ya Song uliendelea kwa kiasi fulani, katika enzi hiyo, ujenzi wa bustani ulianza kustawi. Ujenzi wa bustani ulitilia mkazo muunganisho wa uzuri wa bandia na wa kimaumbile, bustani katika enzi hiyo ilikuwa inapambwa kwa milima bandia, maji, maua na miti ili kuleta mazingira kama ya kimaumbile.
Katika Enzi ya Song kulikuwa na kitabu cha “Ufundi wa Ujenzi wa Nyumba”. Kitabu hiki kinaeleza kanuni za usanifu na ufundi wa ujenzi wa nyumba, ambacho kinaonesha kuwa ujenzi wa nyumba katika Enzi ya Song ulikuwa umefikia kiwango kipya.