Elimu ya Chekechea
Radio China Kimataifa

Elimu ya chekechea ya China ni elimu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 6. Elimu ya chekechea hutolewa katika shule za chekechea na madarasa ya watoto wasiotimiza umri wa kwenda shule. Wizara ya elimu ya China imetunga mwongozo wa elimu kwa watoto wadogo kutokana na uwezo na umaalum wao. Vyombo vinavyotoa elimu ya watoto wadogo vinawafundisha watoto jinsi ya kuhisi mambo, lugha na tabia ya maisha.

Nchini China, shule za chekechea za kawaida huwapokea watoto wenye umri kuanzia miaka 3 hadi 6, baadhi ya shule hizo pia zinawapokea watoto wadogo zaidi. Hivi sasa China kuna shule takriban laki 1 na elfu 50 za chekechea, ni asilimia 30 tu ya watoto wadogo wanapata elimu shuleni, wengine hutunzwa na walezi wao kutokana na umri na hali ya kiuchumi.

Shule za chekechea za China zinagawanyika shule za serikali na za watu binafsi. Zile zinazoendeshwa na serikali zina uzoefu zaidi wa kutoa elimu kwa watoto wadogo, tena zinatoza ada kidogo zaidi, na zile zinazoendeshwa na watu binafsi hutoza ada kubwa, lakini zina sifa zake, na zinaweza kufanya marekebisho kwa urahisi kutokana na mahitaji ya soko. Kutokana na maendeleo ya uchumi wa soko huria, shule za chekechea zinazoendeshwa na watu binafsi zinaongezeka kwa haraka, sasa zimechukua asilimia 30 ya shule zote za chekechea nchini China.