Elimu ya Msingi
Radio China Kimataifa

Elimu ya msingi nchini China inaanza kutoka umri wa miaka 6. Kutokana na sheria ya elimu ya lazima ya China, serikali inawapatia watoto elimu ya lazima bila ada, wanatakiwa tu kulipa gharama za vitabu kiasi cha yuan mia kadhaa hivi kwa mwaka.

Elimu ya msingi ya China ni ya miaka 6, inafundisha masomo ya Kichina, hisabati, sayansi, lugha ya kigeni, maadili, muziki, mchezo wa riadha na kadhalika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, hivi sasa China ina shule zaidi ya laki nne za msingi zenye wanafunzi milioni 120, ambao wanachukua asilimia 98 ya idadi ya watoto wanaotimiza umri wa kwenda shule.

Kwa kuwa elimu ya msingi ni elimu ya lazima, hivyo shule nyingi za msingi nchini China zinaendeshwa na serikali, wanafunzi huwa wanasoma karibu na shule za nyumbani. Hivi sasa idara za elimu za China zinajitahidi kuboresha hali ya shule zenye vifaa duni ili kuwawezesha wanafunzi wote wapate elimu sawa. Katika sehemu Fulani za vijijini ambapo wakazi wanaishi huku na huko, serikali huwapeleka watoto kusoma katika shule za bweni zenye hali bora zaidi.