Elimu ya Sekondari ya Juu
Radio China Kimataifa

Elimu ya sekondari ya juu ya China ni elimu inayotolewa baada ya kumaliza elimu ya sekondari ya chini. Kuna sekondari ya kawaida, sekondari ya ufundi na shule ya kozi maalum. Elimu ya sekondari ya juu ya China si ya lazima, wanafunzi wanatakiwa kulipa ada. Ada hutofautiana kutokana na hali ya kiuchumi ya sehemu mbalimbali, lakini kwa wastani ni yuan elfu mbili hivi kwa mwaka.

Elimu ya sekondari ya juu nchini China huchukua miaka mitatu, ina masomo ya Kichina, hisabati, lugha za kigeni, fizikia, kemia, biolojia, upashanaji habari na kadhalika. Sekondari nyingi za juu huendeshwa na serikali, lakini katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na sekondari za watu binafsi.

Nchini China, wanafunzi wanatakiwa kufanya mtihani wa kujiunga na sekondari ya juu, na kwa mujibu wa matokeo ya mtihani na mapendekezo yao wanapokelewa na shule. Mtihani wa kujiunga na sekondari ya juu hutolewa na idara za elimu za sehemu mbalimbali. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, China ina sekondari za juu zaidi ya elfu 30 zenye wanafunzi milioni 30, ambao wanachukua asilimia 40 ya watoto wa rika moja. Katika miaka ya hivi karibuni, idara za elimu za China zinajitahidi kukuza elimu ya sekondari ya juu ili kutosheleza mahitaji ya wanafunzi kujipatia elimu zaidi.