Hali ya Vyuo Vikuu Nchini China kwa Muhtasari
Radio China Kimataifa

Katika miaka ya hivi karibuni, vyuo vikuu vya kitaifa vya China vimeongeza wanafunzi kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu imeongezeka kwa mara kadhaa kuliko ile ya mwaka 1998, hadi kufikia milioni 20, ambao wanachukua asilimia 17 ya vijana wa rika moja.

Hivi sasa China ina vyuo vikuu zaidi ya 3000, kati ya hivyo, zaidi ya 1300 ni vyuo vikuu vya kawaida, zaidi ya 1200 vinaendeshwa na watu binafsi, vingine ni vya watu wazima. Elimu ya juu nchini China ina madaraja ya vyuo vya shahada, vyuo vikuu, mafunzo ya shahada ya pili na ya udaktari.

Kwa kawaida, wanafunzi wa vyuo vya shahada wanatakiwa kusoma kwa miaka mitatu, na wanafunzi wa vyuo vikuu watasoma kwa miaka minne, na wanafunzi wa shahada ya pili na ya udaktari wanatakiwa kujisoma kwa miaka miwili au mitatu.

Vyuo vikuu vya kitaifa vinatoa mchango mkubwa katika elimu ya juu nchini China, vyuo vikuu vyote vya elimu za mseto na utafiti vinaendeshwa na taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, vyuo vikuu vinavyoendeshwa na watu binafsi vinaongezeka kwa haraka, baadhi ya vyuo hivyo pia vina kiwango kikubwa, lakini bado vina tofauti na vile vya taifa katika sifa na taaluma.