Msikilizaji wetu Xavier Telly Wambwa wa Bungoma Kenya hivi karibuni ametuletea barua pepe akisema, anatumai sisi ni wazima na tunaendelea kuchapa kazi kwa usanifu katika idhaa ya idhaa ya Kiswahili inayosifika huko Mashariki ya Afrika, anasema yeye ni mzima, lakini siku hizi huko aliko anasema kazi ni motomoto sana.
Anasema anapenda kutujulisha kuwa, jumapili moja iliyopita alifurahi sana aliposikia matokeo ya Chemsha Bongo ya kwamba nimepata ushindi pamoja na Bw. Ras Manko Ngogo, ingawa matarajio yake ilikuwa kupata ushindi maalumu ili niweze kupata fursa ya kutembelea mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda.
Anasema ataendelea na juhudi kusikiliza vipindi vya Radio China kimataifa na kuandika maoni, pamoja na kuwa hana muda wa kutosha. Pia anapenda tufahamu kuwa bado anakumbuka Safari yake aliyoifanya hapa China mwezi Mei mwaka wa 2005, na wakati alipokuwa anaandika barua pepe hii, alikuwa anatafakari na kuona jinsi kazi zinavyoendelea kwenye ofisi ya Idhaa ya Kiswahili. Na mwisho anapenda kututakia maisha marefu wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili ya Radio Kimataifa, na ana matumaini kuwa siku moja tutakutana hapa Beijing.
Tunakushukuru sana Bw Xavier Telly Wambwa kwa barua pepe yake. Tunafurahi kupata barua yake, lakini hata hivyo tunasikitika kuwa mawasiliano kati yetu yamepungua, lakini tunaweza kukuelewa kwa sababu umetuambia kuwa umekuwa na pilika nyingi katika kazi. Tunakupongeza sana wewe na Bw Ngogo kwa kupata nafasi ya kwanza kwenye shindano la chemsha bongo.
Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za Kiarabu katika barua yake anasema, katika mataifa tajiri ya Ghuba ya Uajemi kama huko aliko, mtandao ya Internet umekuwa ni jambo la kawaida katika maisha ya wakazi wote wa nchi hiyo kama yeye msikilizaji wetu anayeishi huko mjini Dubai, hivyo imekuwa ni rahisi sana kwa yeye kutumia njia ya Internet kusikiliza matangazo ya Idhaa mbalimbali za Kiswahili za Kimataifa ikiwemo Redio China Kimataifa, kwa kupitia tovuti tena kwa wakati wowote ule anaopenda.
Anasema hata hivyo lakini si rahisi njia hii kutumiwa na wasikilizaji wenzake wengi wanaoishi katika nchi za Afrika Mashariki, hususan nchini Tanzania ambako bado gharama za matumizi ya Internet ni kubwa, na hata internet haijaweza kusambaa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa urahisi. Akiwa msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kwa karibu miaka 19 sasa, maoni yangu juu ya usikivu wa matangazo yenu nchini Tanzania ni kwamba juhudi zinapaswa kuchukuliwa haraka iwezekanavyo, ili kuboresha usikivu wa vipindi vyetu kama ni msingi mkuu wa kuboresha mahusiano mazuri kati ya Redio China Kimataifa na wasikilizaji wake.
Anasema yeye binafsi anaamini kuwa mafanikio ya Redio China Kimataifa nchini Tanzania yataweza tu kufanikiwa ikiwa matangazo yenu yatawafikia nyema walengwa, kwa vile tayari ndugu zetu wa Kenya wamekuwa wakinufaika na usikivu mzuri wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kupitia Shirika la Utangazaji na KBC kwa kupitia mtambo wa 91.9 FM, ni vyema juhudi hizo sasa zikiimarishwa Tanzania.
Bila shaka Watanzania ambao sio tu kama nao ni sehemu kubwa kabisa ya wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa tangu kuasisiwa kwake, na Idhaa zote za Kiswahili za Kimataifa hapa duniani, nao pia wana hamu ya kuona kwamba Redio China Kimataifa inafanya juhudi za kupeperusha matangazo yake kwa njia nzuri kabisa itakayowaridhisha wasikilizaji wake kama vile inavyofanya nchini Kenya.
Hatuwezi kukwepa ukweli kwamba yote hayo yanaweza tu kufanikiwa ikiwa mashirika ya utangazaji ya Tanzania ikiwa ya binafsi au ya serikali, yataonesha kuwa kwao tayari kushirikiana na Redio China Kimataifa katika swala hilo ili kufikia malengo yanayokusudiwa. Juhudi za pande mbili zinapaswa kuchukuliwa hivi sasa ili kuondoa kilio cha wasikilizaji wa Redio China Kimataifa nchini Tanzania, ambao wanaendelea kusikitika na kuhuzunika juu ya usikivu usioridhisha wa matangazo yetu. Anasema ni matumaini yake makubwa kwamba, wahusika wa Idhaa hii wataweza kulishuhulikia swala hili kwa haraka.
Tunakushukuru sana Bw Mbaruk Msabah kwa barua pepe yako ambayo imebeba malalamiko ya wasikilizaji wetu. Unayosema yote ni kweli na hali hii pia haitufurahishi, si wewe tu, hata wasikilizaji wengine pia wamelalamikia hali hiyo. Lakini tunapenda wasikilizaji wetu mfahamu kuwa tumefanya ziara (tatu) nchini Tanzania, tumeonana na wakuu wa vyombo binafsi na vyombo vya Taifa ikiwa ni pamoja na Tanzania bara na Tanzania visiwani, ili tuweze kuwa na utaratibu kama uliopo Kenya. Kimsingi, makubaliano yamefikiwa kati ya Radio China kimataifa na upande wa Tanzania bara na Visiwani. Kwa upande wa Zanzibar tumefikia hatua nzuri na tuna makubaliano yamesainiwa, kinachosubiriwa ni utekelezaji, ni muda kiasi tu unahitajika ili utekelezaji uanze, kwa upande wa Tanzania Bara tumefanya mazungumzo na bado yanaendelea, Huenda wasikilizaji wetu mnafahamu kuwa huko Tanzania kumekuwa na mabadiliko ya muundo wa uongozi wa Radio Tanzania, mambo yakitengemaa utekelezaji wa makubaliano utakuwa wa haraka zaidi. Tunaomba wasikilizaji wetu mvute subira kidogo, sisi pia tuna nia thabiti ya kuondoa hali hiyo.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-25
|