Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-29 15:47:54    
Barua 0127

cri

Msikilizaji wetu Yaaqub Saidi Idambira ambaye barua zake huhifadhiwa na Msikiti wa Jamia Kakamega Kenya ametuandikia barua akianza kwa salamu za heri na Baraka kwa watayarishaji wa vipindi na watangazaji wote wa Radio China Kimataifa, akitarajia kuwa sisi sote tu wazima, tukiendelea na kuchapa kazi ya kuwahudumia wasikilizaji kwa matangazo na vipindi vyetu vya kuelimisha, kufahamisha na hatimaye kuwaburudisha. Kwa hakika hali yake ni njema huku akiendelea kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Anasema kwa mara nyingine Radio China Kimataifa itaingia kwenye vitabu vya historia ya kumbukumbu kwa kwenda hatua mbele katika fani hii ya utangazaji na utoaji wa habari, siku za mbele itaanzisha ushirikiano na Shirika la utangazaji la Uganda, kama njia mojawapo ya kuboresha na kuimarisha matangazo ya vipindi kwa wasikilizaji wake kote duniani.

Bwana Yakubu pia anasema ni dhahiri kwamba taifa la China ni taifa lenye heri njema na mapenzi makubwa kwa Jumuiya ya Afrika mashariki na bara la Afrika kwa jumla, kwani kwa wakati mwingine taifa la China limeonesha kuwa tayari kutoa msaada wa mkono wa ushirikiano, kwa kutuma wataalamu wake wenye taaluma ya ujenzi wa barabara, madaraja, viwanja vya michezo, hospitali na miundo mbinu mingine mbalimbali barani Afrika. Vilevile sekta ya habari haijaachwa nyuma katika kuimarishwa na kupewa kipaumbele na serikali ya Jamhuri ya watu wa China, kwani kumefanywa ziara ya kubadilishana maoni kati ya wadau katika sekta hii ya utangazaji hasa wakuu wa mashirika ya habari ambao wamefanya ziara nchini China toka barani Afrika kujionea namna China ilivyopata mafanikio katika mambo haya ya habari.

Pia waandishi wa habari wa bara la Afrika walipata fursa ya kuzuru China na kujifunza mengi hasa mbinu na mikakati ya kuboresha utendaji wao wa kazi. Kwa mustakabali huu anatoa changamoto kwa wadau wa mambo ya habari wa barani Afrika kutumia ujuzi wao waliopata nchini China kuboresha na kuimarisha mahusiano yao na wachina wadau wengine. Ni matumaini yake kwamba uongozi wa Radio China Kimataifa utaendelea na juhudi zake za kufungua mlango kwa mataifa ya Afrika ili kudumisha na kujenga uhusiano mzuri na wasikilizaji wake walio wengi barani Afrika. Anasema hongera sana Radio China Kimataifa kwa kusikika barani Amerika mpaka kwenye nchi za barani Afrika, na anatutakia kila la heri.

Tunamshukuru sana Bw. Yaaqub Saidi Idambira kwa barua yake inayoeleza ushirikiano na urafiki kati ya China na nchi za Afrika. Barua yake pia imetukumbusha mengi tuliyokuwa tukitangaza kuhusu vikundi vya wanahabari vilivyokuja hapa China mwaka jana kutoka barani Afrika, kwenye nchi za Kenya, Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda, visiwani Shelisheli na kadhalika na sisi kupata bahati ya kufanya mahojiano nao. Barua yake kweli inatuonesha kuwa yeye alikuwa makini zaidi wakati wa kusikiliza, na ametutia moyo ili tuendelee kuchapa kazi ili kuwahudumia vizuri zaidi wasikilizaji wetu popote walipo.

Na msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sharif wa S.L.B 172 Bungoma nchini Kenya anasema katika barua aliyotuandikia kuwa, kutokana na upendo alionao kwa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa anatuomba wahariri, watangazaji na wasikilizaji wote kumwia radhi kwa kimya changu cha muda mrefu. Katika siku chache hizi amekuwa anajiona kama amepungukiwa na kitu fulani, na sababu ya kijisikia hivyo inatokana na kutopata jarida lolote kutoka idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, iwe ni China Today au China Pictorial. Anauliza ni kwa nini? kwani majarida hayo yanamsaidia sana kufahamu mengi kuhusu China na wasomaji wa mjini Bungoma wanaotembelea maktaba ya kijamii ya Bungoma wanavutiwa sana kuweza kufahamu mengi kuhusu China.

Bwana Mutanda anaendelea kusema hakuna barua atakayoandika akose kukumbushia safari yake aliyoifanya nchini China mwaka mmoja uliopita, kwa kweli alipata kuiona nchi nzuri ya China na yenye miundo mbinu bora kabisa, na wananchi wakarimu sana kwa wageni. China ina sehemu nzuri sana na kubwa za utalii ukiwemo ukuta mkuu wa Beijing "ama kweli ni ukuta mkuu na mrefu duniani". Akiitazama China ilivyokuwa ikiendelea kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki mwaka jana alifikiri kila kitu kimekamilika, lakini alipigwa na butwaa kuambiwa kuwa maandalizi bado yanaendelea.

Pia anasema kutokana na habari anazopata msikilizaji wetu huyu kupitia idhaa ya Kiswahili ya Radio China kuhusu maandalizi ya michezo ya Olimpiki, ni matumaini yake kuwa wote watakaopata bahati ya kuhudhuria michezo hiyo nchini China watakuwa wamefika katika nusu mbingu. Hivyo anawaomba wananchi wote wa nchi za Afrika watembelee China hasa mwaka 2008, kuna usalama wa kutosha na ukomavu wa kisiasa. Anamalizia barua yake kwa kuwatakia wote heri na baraka ya mwaka mpya wa 2008.

Na kwenye barua pepe aliyotuandikia, Bw. Mutanda Ayub anasema uhusiano uliopo kati ya China na nchi za Afrika unazidi kuendelea na kuleta maendeleo kwa pande zote. Fursa ya maendeleo kama hii kweli inastahili sifa na pongezi. Na yeye binafsi anasema anatambua jinsi kazi zetu za kutangaza habari zinazohusu maendeleo ya China na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika. Na kwa kuwa yeye alikwishapata nafasi ya mshindi maalum, anaona hataweza kuja kushuhudia michezo ya Olimpiki kwa sababu nafasi hiyo anataka wapate wengine ambao bado hawajatembelea China. Na vilevile anafahamu kuwa kutokana na pilika nyingi za kazi tulizonazo, sio rahisi kwa sisi kuwatembelea wasikilizaji wetu wa Kenya kwa sasa. Anasema tuombe mungu labda baadaye yatawezekana.

Anasema hata hivyo itakuwa vigumu kwake kumaliza barua yake bila kugusia yale yaliyoikumba Kenya. Wananchi wa Kenya walikumbwa na vurugu ambazo ziliwafanya wachelewe kupata hata barua na kusikiliza vipindi kutoka China. Lakini baada ya kuwa na nafasi ya kusikiliza matangazo, walifarijika kusikia kuwa vurugu zimetulia, na hali baada ya uchaguzi inaelekea kuwa shwari.

Tunamshukuru sana Bw. Mutanda Ayub Sharif kwa barua yake iliyotuelezea hisia zake za dhati kwa Radio China Kimataifa, ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano. Siku hizi kutokana na msukosuko wa kisiasa nchini Kenya, sisi sote tuna wasiwasi mkubwa, kila mara tunawatakia wasikilizaji wetu na wananchi wote wa Kenya waishi katika mazingira yenye usalama, amani na utulivu, ili kufanya juhudi za kujenga nchi nzuri.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-29