Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-15 19:00:00    
Barua 0415

cri

Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi cha sanduku la barua. Leo kwanza tunawaletea barua tulizopata kutoka kwa wasikilizaji wetu. Msikilizaji wetu Mogire Machuki wa Kijiji cha Nyankware SLP 646 Kisii Kenya ametuandikia barua akianza kwa salamu tele za heri ziwafikie wasikilizaji na wafanyakazi wa Radio China Kimataifa. Anasema huko Kisii Kenya yeye na wasikilizaji wengine wako salama, baada ya hali ya taharuki ambayo ilichochewa kwa kiasi fulani na matokeo ya kura ya urais kutokana na uchaguzi mkuu uliomalizika rasmi mwaka jana Desemba kuondolewa, na sasa yeye na wakenya wengine wanaendelea na shughuli zao za kila siku.

Yeye binafsi anaamini kuwa kuwasili nchini Kenya mpatanishi wa kimataifa Bw. Koffi Annan, bila shaka kulionesha kuwa suala la uchaguzi lilikuwa na utatanishi. Anaelewa kuwa wachina walikuwa pamoja na wakenya, kwa kuwa China na Kenya ni mataifa mawili ambayo yamekuwa na uhusiano wa karibu kwa zaidi ya miaka 600 tangu mwanabahari kutoka China Zheng He alipowasili kwenye pwani ya Kenya kwa merikebu. Anasema anaishukuru serikali kuu ya China kuwasaidia watu walioathiriwa vibaya na mgogoro huo.

Bwana Machuki anaongeza kuwa, ni muhimu sana amani kurejea nchini Kenya. Huu ni mwaka muhimu sana kwa nchi ya Kenya kwa vile Michezo ya Olimpiki ya Beijing inakaribia, Kenya inasifika kote duniani, kama taifa pekee barani Afrika ambalo lina idadi kubwa la wakimbiaji wa masafa marefu. Pia alisema walikuwa wanaomba sana mzozo ambao uliikumba Kenya uishe haraka i, ili watakaofuzu kuiwakilisha Kenya kwenye fainali hizi wawe wa muda wa kutosha wa kufanya mazoezi, ili wawe na nafasi nzuri ya kuzoa medali wakati utakapowadia, macho yote ya dunia kwa sasa yameelekezwa Beijing na taarifa ambazo amezikusanya mpaka sasa ni kwamba, Jamhuri ya watu wa China tayari kwa tafrija hii ya kuandaa fainali hizi, fainali ambazo zitakuwa za kipekee kutokana na teknolojia ya kisasa ambayo umetumika kujenga viwanja vya hali ya juu. Anaona viwanja hivi vitakuwa muhimu sana kwa wachina baada ya kukamilika kwa Michezo ya Olimpiki. Mwishoni Bw. Machuki anaitakia China mwaka wa 2008 uwe na mafanikio.

Barua hii tumechelewa kuipata hivyo ameeleza hali ya hapo kabla ya Kenya, hivi sasa hali ya nchini Kenya ni shwari, tuna imani kuwa wakenya akiwemo Bw. Mogire Machuki na watu wa familia yake wanaendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida. Na wachezaji wa Kenya watakaokuja China kushiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 hakika wanajiandaa na kujitahidi kufanya mazoezi ili kufuzu kuiwakilisha Kenya kwenye michezo ya Olimpiki.

Msikilizaji wetu Dennis Ombese wa sanduku la posta 8 kutoka Kisii Kenya ametuandikia barua akianza kwa salamu kutoka Kisii-Kenya. Alisema anapenda kuwapongeza wasikilizaji walioshiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo kuhusu "Sichuan maskani ya Panda". Alisema walijitahidi kadiri ya uwezo wao na wakajipatia ushindi ambao wanastahili kupongezwa, kwani hii ni njia moja ya kuboresha matangazo ya Radio China kimataifa na kuifahamu nchi ya China. Anaongeza kuwa, bila matangazo ya Radio China Kimataifa wasingeweza kuifahamu China, lakini sasa wameweza kuifahamu China kama nchi ambayo ina vivutio vya kila aina, kwa mfano mkoa wa Sichuan ambao ni maskani ya Panda ni kivutio cha watalii ambao wataizuri China. Bw. Ombese anataka kuifahamu China vizuri, kwa hiyo anaona ni bora asikilize matangazo ya Radio China kimataifa. Anawatakia kila la heri wasikilizaji na wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa katika maisha yao, na anapendelea kutuhimiza tuwafahamishe mengi zaidi kuhusu China na vivutio vyake ambavyo vinapendwa. Mwishoni anapenda kuwakumbusha wasikilizaji wa Radio China Kimataifa waendelee na ushirikiano na watoe mapendekezo ambayo yataweza kuiboresha.

Msikilizaji wetu mwingine Bw Paul Mungai Mwangi wa sanduku la posta 69 Injinia North Kinangop, Kenya ametuletea salamu akisema, ni matumaini yake kuwa wafanyakazi na wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wote hawajambo. Anasema anaomba kupendekeza kwamba Radio China Kimataifa ianzishe kipindi kipya kinachoitwa "Sauti za wasikilizaji". Kwa maoni yake kipindi hiki kitawawezesha wasikilizaji kuongea moja kwa moja redioni kwa njia ya simu. Wasikilizaji wawili kila siku wanaweza kupewa fursa hii kuzungumzia mada mbalimbali kuhusu uchumi, utalii, utamaduni na jamii, na mwishoni mwa mahojiano kila mmoja apewe nafasi ya kutuma salamu kwa wasikilizaji watatu.

Pia anapenda kuwajulisha wahifadhi wa kumbukumbu za klabu za wasikilizaji wa hapa CRI kuwa sasa amebadilisha namba yake ya simu ya mkononi aliyowasilisha kwenye kidadisi. Mwishoni anaomba kuwasalimia wafuatao Baba na mama Mwangi Gichimu na Margaret Muthoni wa Injinia, Kenya, Geoffrey Njereka wa Mkwanjuni, Tanzania, Mutanda Ayub wa Bungoma, Kenya, Ras Franz Manko Ngogo wa Tarime-Mara, Tanzania, Mogire Machuki wa Kisii, Kenya, Mbarouk Msabah wa Dubai na ujumbe kwa hao aliowasalimu anasema utamu wa Salamu ni kusalimiana.

Tunawashukuru wasikilizaji wetu Dennis Ombese na Paul Mungai Mwangi kwa barua zao za kueleza maoni yao kuhusu vipindi vyetu, maoni yao ni mazuri, kwa mfano kuhusu kuanzisha kipindi cha "Sauti ya wasikilizaji", mwaka jana tulikuwa na kipindi kama hicho, lakini ni vigumu kwetu kudumisha kipindi hiki, kwani kila mara, tulikuwa tunaona vigumu kupata maoni ya wasikilizaji, kutokana na nguvu ya idhaa yetu kwa hivi sasa, hatuna uwezo wa kutafuta na kupata maoni ya wasikiliza kila mara, hivyo, tuliweza tu kuandaa vipindi wakati tulipopata maoni ya wasikilizaji. Maoni ya wasikilizaji wetu hakika tutazingatia kwa makini, na tutaendelea na juhudi za kuboresha vipindi vyetu.