Mwezi Mei, duniani yote ilielekeza macho yake kuelekea Mjini Beijing kwa sababu ya tukio kubwa ya kihistoria iliyokuwa ikiendelea katika mji huo mkuu wa China. Serikali mbalimbali na mashirika ya kimataifa yalikuwa hapa kushuhudia kuzaliwa kwa mpango wa maendeleo wa Mkanda Mmoja Njia Moja.
Maafisa muhimu kutoka Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha ulimwenguni IMF walikuwa hapa pia. Bila kumsahau kiongozi wa Urusi Vladimir Putin.
Kutoka Afrika, Kenya na Ethiopia hawakuwakilishwa na wengine kando na viongozi wao wa taifa. Wao walikuwa miongoni mwa viongozi 29 duniani walioalikwa na Rais wa China Xi Jinping kuhudhuria kikao hicho cha kwanza kabisa kuwahi kufanyika. Lakini hawakuwa peke yao, kwani kila mmoja alifika hapa na ujumbe spesheli wa mawaziri na wataalam.
Tanzania iliwakilishwa na waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Rais Uhuru Kenyatta alikuwa akiandamana na mawaziri wa Usafiri, Nishati, Viwanda na Mambo ya Nje. Mkuu wa sheria na mshauri mkuu wa serikali wa nchi hiyo Profesa Githu Muigai pia alijumuika katika baraza hilo.
Kwa mujibu wa waziri wa usafiri James Macharia, ambaye wizara yake inasimamia miradi ya miundombinu, Kenya ilibahatika sana kwa kualikwa kushiriki katika baraza hilo. Kwa maoni yake, ishara ile ilikuwa ya kihistoria katika kila nyanja.
"Kimsingi inaonyesha aina ya mafanikio ambayo tumeafikia kama taifa, kwa kuwa na ufahamu wa kina wa mambo kwa mujibu wa masuala yanayohusiana na miundombinu." Alisema
Waziri huyo alipongeza uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa kuandaa kongamano hilo ambalo alikitaja kuwa tukio muhimu katika majadiliano kuhusu njia ambazo nchi zinaweza kushirikiana na kujenga ushirikiano kupitia mapendekezo ya Mkanda Mmoja Njia Moja.
Hata hivyo, Macharia alikuwa mwepesi kusema kwamba Mkanda Mmoja Njia Moja haikuwa wazo tena bali ni mfumo hai. Aidha alisimulia jinsi swala la maendeleo ya miundombinu katika Afrika Mashariki ilizungumziwa kwa mapana na marefu wakati wa mazungumzo ya pamoja ya mataifa husika 68 na mashirika ya kimataifa ambayo hadi sasa yamejiunga katika mpango huo.
"Kwetu sisi hii si dhana tena kwani tayari tumefanya maendeleo ya miundombinu ili kudhihirisha kwamba mfumo wa Mkanda Mmoja Njia Moja ni hai na inaendelea." Alisisitiza.
Alisema hii inaonekana kupitia ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR inayounganisha Mombasa na Nairobi. Reli hiyo iliyogharimu mabilioni ya pesa na ambayo itazinduliwa hivi karibuni, unajengwa kwa msaada kutoka serikali ya China.
"Katika muda wa siku 20 tutakuwa na uzinduzi mkubwa zaidi kuwahi kufanyika ndani ya miaka 100 iliyopita katika Afrika. Hiyo ni mradi wa SGR ambayo tumekuwa na shauku ya kusubiri kumalizika kwake." Macharia alisema.
Akihutubia waandishi wa habari mjini Beijing kabla ya kusafiri kurudi Nairobi baada ya mkutano wa BRF, waziri huyo wa usafiri alisema ana Imani kwamba Kenya itashuhudia mabadiliko makubwa zaidi kupitia mfumo wa Mkanda Mmoja Njia Moja.
"Ni dhihirisho kuwa tuna mafanikio ambayo yanaweza kuonekana. Ni dhahiri kwa mtu yeyote kuona na kwa hiyo sisi tuna bahati ya kuwa sehemu ya huu mpango." Macharia alisema.
Kukamilika kwa SGR kulingana na Macharia kutainua hadhi ya taifa lake katika kanda, huku akidokeza kuwa nchi jirani zitafaidika kupitia miradi ya ujenzi wa barabara imara na reli zinazofanywa nchini Kenya.
"Tumeweka mfano wa kuigwa, tutaendelea kuwa picha nzuri katika suala la maendeleo ya kikanda katika miundombinu." Alisema
Waziri huyo alipongeza Rais Kenyatta mahsusi kwa kuwa kipaumbele kwa ujenzi wa reli ya kisasa Kenya, ambayo sasa inasubiri upanuzi kuelekea miji ya Kisumu na Malaba kabla ya kuenezwa hadi Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.
Kenya, Tanzania na Ethiopia zinatarajia kufaidika kwa kiasi kikubwa kutoka bajeti ya bilioni 8.7 dola za marekani ambazo zimetengwa na serikali ya China ili kutoa misaada kwa miradi katika nchi ambayo sasa ni sehemu ya Mkanda Mmoja Njia Moja.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |