Timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa yasema kundi la IS lilifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wayazidi nchini Iraq
2021-05-11 16:29:01| Cri

Kiongozi wa timu ya Umoja wa Mataifa inayochunguza uhalifu wa kundi la IS nchini Iraq, Karim Khan amesema jana kuwa, kuna ushahidi wa wazi na wa kuaminika kuwa kundi hilo la kigaidi lilifanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa kabila la Yazidi nchini Iraq.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja huo, Khan amesema kutokana na uchunguzi huru na usio na upendeleo, unaoendana na vigezo vya kimataifa na Umoja wa Mataifa, kuna ushahidi kuwa uhalifu uliofanywa dhidi ya watu wa kabila la Yazidi ni sawa na mauaji ya kimbari.

Amesema timu yake imewatambua wahusika halisi ambao wanawajibika na uhalifu dhidi ya kabila hilo, na kuongeza kuwa, maelfu ya wanaume, wanawake na watoto waliuawa vibaya na wapiganaji wa kundi la IS pale walipokataa kukana dini zao.

Khan amesema uhalifu wa IS dhidi ya kabila la Yazidi umeonyeshwa katika vitendo vya uhalifu dhidi ya jamii hiyo, ikiwemo, kuuawa, utumwa, utumwa wa ngono, na uhalifu dhidi ya watoto.