China bado inaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watu duniani
2021-05-11 17:09:16| Cri

China bado inaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watu duniani_fororder_VCG111329427427

Idara ya Takwimu ya China leo imetoa Takwimu muhimu kuhusu Sensa ya saba ya idadi ya watu ya China, na kuonesha kuwa idadi ya watu wa China imezidi bilioni 1.4, na China bado ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Katika miaka 10 iliyopita, idadi ya watu wa China imekuwa ikiongezeka kwa kasi ndogo.

 

Kutokana na takwimu hizo, idadi ya watu wa China imefikia bilioni 1.41, ambayo imeongezeka kwa milioni 72 ikilinganishwa na mwaka 2010, na wastani wa kiwango cha ongezeko la idadi ya watu umepungua kwa asilimia 0.04 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2000-2010.

Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu ya China Bw. Ning Jizhe anaona kuwa, kwa mujibu wa matokeo ya sensa hiyo, hivi sasa idadi ya watu wa China inaendelea kushika nafasi ya kwanza duniani, na kuzitaja sababu tatu kuu za hali hiyo:

 “Kwanza, idadi ya watu wa China inadumisha ongezeko. Kwani China ina watu wakiwemo wanawake wenye umri mwafaka wa uzazi zaidi ya milioni 300, ambao wanaweza kudumisha idadi ya watoto zaidi ya milioni 10. Pili, marekebisho ya sera ya uzazi yamepata ufanisi mzuri. Baada ya utekelezaji wa sera za kuhimiza uzazi, idadi ya watoto inarejea kwa kasi. Tatu, makadirio ya umri wa watu kuishi yanazidi kuongezeka.”

Bw. Ning anaona kuwa kutokana na hali ya jumla, raslimali ya nguvu kazi ya China bado ni kubwa. Anasema:

 “Takwimu za sensa hiyo pia zimeonesha kuwa idadi ya watu wenye umri mwafaka wa kufanya kazi ni milioni 880, na wastani wa umri wa idadi ya watu ni 38.8. Takwimu zilizotangazwa hivi karibuni na Marekani zimeonesha kuwa wastani wa umri wa wamarekani ni 38, ambayo inalingana na China.”

Takwimu pia zimeonesha kuwa, idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi nchini China imefikia asilimia 18.7, na wale wenye umri wa miaka 65 na zaidi imefikia asilimia 13.5. Bw. Ning anaeleza kuwa, ongezeko la idadi ya wazee ni mwelekeo muhimu wa jamii, pia ni hali ya kimsingi ya China ndani ya muda mrefu ujao, ambayo pamoja na kuwa ni changamoto, lakini pia italeta fursa.