Chanjo ya Sinovac yapunguza dalili za COVID-19 kwa wahudumu wa afya nchini Indonesia kwa asilimia 94
2021-05-12 18:32:36| Cri

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya nchini Indonesia umeonyesha kuwa, chanjo ya virusi vya Corona iliyotengenezwa na Kampuni ya Sinovac Biotech ya China imepunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya dalili za virusi vya Corona kwa wahudumu wa afya nchini humo kwa asilimia 94.

Kiongozi wa timu ya watafiti hao Pandji Dhewantara amesema leo kuwa, utafiti uliofanywa kuanzia Januari 13 mpaka Machi 18 mwaka huu umehusisha wahudumu wa afya 128,290 ambao hawakupata maambukizi ya virusi vya Corona, na kwamba hitimisho la utafiti huo lilifanyika baada ya wahudumu hao kupata dozi ya pili ya chanjo hiyo.

Pia utafiti huo ulihitimisha kuwa, chanjo ya virusi vya Corona ya Sinovac ina ufanisi wa asilimia 96 katika kuwaepusha wahudumu wa afya kulazwa kutokana na kuambukizwa kwa virusi hivyo, na asilimia 98 ya ufanisi katika kuzuia vifo vinavyotokana na virusi hivyo.