Shughuli za mazoezi ya kukabiliana na maafa zafanyika katika sehemu mbalimbali kote nchini China
2021-05-12 17:05:43| Cri

Leo ni siku ya 13 ya kukinga na kupunguza maafa nchini China, kauli mbiu ya mwaka huu ni “kuepukana na kupunguza hatari za maafa, na kuimarisha msingi wa kuhimiza maendeleo kwa usalama”. Hivi karibuni, shughuli za kukinga maafa mbalimbali ikiwemo mafuriko, moto misituni na matetemeko ya ardhi zimefanyika katika sehemu mbalimbali kote nchini, ili kuimarisha hatua za dharura za kukabiliana na maafa, na uwezo wa wananchi wa kukabiliana na maafa.

China ni moja kati ya nchi zilizoshuhudia majanga mabaya zaidi ya kimaumbile duniani. Takwimu zimeonesha kuwa, tokea karne ya 21, wastani wa athari za kifedha kila mwaka kutokana na majanga ya kimaumbile yaliyotokea nchini China umezidi RMB yuan bilioni 300, sawa na dola za kimarekani bilioni 46, na kila mwaka watu milioni 300 wanaathirika kutokana na majanga. Kutokana na hali hii, mkurugenzi wa Idara ya usimamizi wa hali ya hatari na kupunguza maafa iliyo chini ya Wizara ya usimamizi wa hali ya dharura ya China Bw. Chen Sheng ameeleza kuwa, ili kuongeza uwezo wa jamii nzima wa kukabiliana na majanga ya kimaumbile, kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kukinga na kupunguza maafa. Anasema:

 “Majanga ya kimaumbile yanaweza kuleta hatari kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Lengo la shughuli za mwaka huu ni kuwaelekeza wananchi kuelewa vizuri wazo la kukabiliana na hali ya hatari, kuhamasisha nguvu mbalimbali za jamii kushiriki katika kinga na mapambano dhidi ya maafa, ili kupunguza kadiri iwezavyo hatari za maafa na athari zinazotokana na maafa, na kuhimiza ongezeko la uwezo wa jamii wa kukinga na kupunguza maafa.”

Shule moja ya sekondari ya wilaya ya Jinxian mkoani Jiangxi ilifanya mazoezi ya kukabiliana na tetemeko la ardhi, ili kuwasaidia watoto wafahamu utaratibu wa kukabiliana na hali ya dharura, na ukosefu wa salama ndani ya muda mfupi. Mkurugenzi wa Idara ya kupunguza maafa katika wilaya ya Jinxian mkoani Jiangxi Bibi Zhang Suping anasema:

 “Jamii yote inazingatia sana kupunguza maafa, haswa ufahamu wa watoto kuhusu elimu husika. Shughuli hizi zitafanyika katika mitaa, makampuni na jamii, ili kuwafanya watu wote wafahamu umuhimu wa kupunguza maafa, na kulinda usalama wa maisha na mali.”