China yapenda kunufaika kwa pamoja na makampuni ya kigeni kutokana na fursa mpya katika zama mpya
2021-05-13 17:02:54| Cri

Ofisa wa Kamati ya Maendeleo na Mageuzi ya China Gao Jian leo mjini Shanghai amesema kuwa, makampuni ya kigeni yana umuhimu kwa maendeleo ya uchumi ya China, na China inapenda kushirikiana na makampumi mengi ya kigeni yakiwemo ya Marekani kunufaika kwa pamoja kutokana na fursa mpya katika zama mpya.

Shanghai ni mji unaoongoza miji mingine nchini China katika kufungua mlango. Takwimu zimeonesha kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, makampuni ya kigeni mjini humo yameweka rekodi mpya kwa kuchangia robo ya pato la taifa GDP, theluthi moja ya mapato ya kodi, na theluthi mbili ya uagizaji na uuzaji wa mizigo nje, na kutoa moja ya tano ya nafasi zote za ajira. Licha ya janga la virusi vya Corona, mwaka jana uwekezaji wa kigeni mjini Shanghai uliongezeka na kuzidi dola za kimarekani bilioni 20, likiwa ni ongezeko la asilimia 6.2, na kuweka rekodi mpya katika historia, hali ambayo imeyafanya makampuni ya kigeni mjini Shanghai yawe na imani kubwa juu ya mustakabali wa maendeleo mazuri ya uchumi endelevu kwa mji huo na China.

Ili kuhimiza kwa ufanisi zaidi makampuni ya Marekani nchini China kujiunga na muundo mpya wa maendeleo ya China, maofisa wa Kamati ya Maendeleo na Mageuzi ya China walifanya mawasiliano na wawakilishi 92 wa Makampuni 75 ya Marekani nchini China pamoja na mashirikisho ya wafanyabiashara. Naibu mkurugenzi wa Idara ya mambo ya kimataifa chini ya kamati hiyo Bw. Gao Jian anasema:

 “Maendeleo na mafanikio ya Shanghai yameonesha kidhahiri kuwa, mageuzi na ufunguaji mlango ni njia ya lazima tunayopaswa kushikilia siku zote, na kwamba ni njia ya kustawisha taifa na kuwanufaisha wananchi, na makampuni ya kigeni yakiwemo yale ya Marekani ni sehemu muhimu za lazima katika maendeleo ya uchumi wa China.”

Bw. Gao amesisitiza kuwa, China itafungua wazi zaidi mlango wake katika siku zijazo. Katika kipindi cha “Mpango wa 14 wa Maendeleo wa Miaka Mitano”, China itafuata wazo la kufungua mlango, kushirikiana, kushikamana na kunufaika kwa pamoja, kushikilia kupanua ufunguaji mlango kwa pande zote, ili kulifanya soko la China liwe soko la dunia, la kunufaika kwa pamoja, na la watu wote. Bw. Gao anasema:

 “Uchumi wa China umeshiriki kwa kina katika uchumi wa dunia. Tunapenda kunufaika kwa pamoja na fursa mpya katika zama mpya na makampuni mbalimbali ya kigeni yakiwemo yale ya Marekani, ili kujenga mustakabali mzuri zaidi kwa pamoja.”