Rais wa China akagua mradi wa kuhamisha maji kutoka kusini hadi kaskazini
2021-05-14 16:53:33| cri

 

 

Rais Xi Jinping wa China ambaye yuko kwenye ziara ya ukaguzi mkoani Henan, jana alikagua mradi wa kuhamisha maji kutoka sehemu za kusini hadi kaskazini ulioko katika wilaya ya Xichuan mkoani humo. Rais Xi aliwashukuru wajenzi na vibarua wahamiaji wanaojenga mradi huo kutokana na mchango wao kwa mpango wa taifa wa kutumia vizuri rasilimali ya maji.

Kituo cha kwanza kilichokaguliwa na rais Xi ni mwanzo wa mfereji wa Taocha, ambao unaunganisha bwawa la Danjiangkou na mfereje mkuu wa kusafirisha maji, na ni “bonde kuu” la sehemu ya katikati ya mradi wa kuhamisha maji kutoka kusini hadi kaskazini. Mradi huo ambao ni mradi mkubwa zaidi wa kuhamisha maji duniani ulianza kubuniwa mwaka 1952, na kukamilika mwaka 2014. Hadi mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, kupitia mradi huo, takriban maji mita bilioni 42 yamehamishwa kutoka sehemu za kusini zenye mvua nyingi, na kupelekwa sehemu za kaskazini ikiwemo mikoa ya Henan na Hebei, na miji ya Beijing na Tianjin, ambayo inakumbwa na upungufu wa maji kwa muda mrefu, na kunufaisha zaidi ya watu milioni 120.

Kutokana na mradi huo, watu wengi walihamia katika wilaya ya Xichuan. Takwimu zinaonesha kuwa, karibu watu laki nne wa wilaya hiyo walihamia kutokana na ujenzi wa bwawa na mifereji. Rais Xi amekagua kijiji cha Zouzhuang cha wilaya hiyo, akisema huu ni mwaka wa 100 tangu kuasisiwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China, na lengo kuu la Chama hicho ni kuwapatia watu maisha bora. Amewashukuru wajenzi na vibarua wahamiaji walioshiriki katika ujenzi wa mradi wa kuhamisha maji kutoka kusini hadi kaskazini, amesema, “Ninafuatilia kwa karibu ujenzi na uendeshaji wa mradi wa kuhamisha maji kutoka sehemu ya kusini hadi kaskazini. Pia ninafuatilia sana maisha yenu nyie wahamiaji kutokana na mradi huo. Mmetoa mchango mkubwa kwa ajili ya watu wengine kuweza kupata maji safi na ya kutosha. Mnastahili shukrani zetu. Nawatakia maisha bora na ustawi zaidi.”