Uchumi wa China waimarika zaidi katika mwezi Aprili
2021-05-17 18:30:04| CRI

 

Takwimu zilizotolewa leo na Idara Kuu ya Takwimu ya China zinaonesha kuwa, katika mwezi Aprili, mahitaji na uzalishaji vimeendelea kuongezeka, ajira na mfumuko wa bei vimedumisha utulivu, na uchumi umeendelea kufufuka na kuimarika.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa katika mwezi uliopita, ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huu, ongezeko la thamani ya viwanda nchini China ilikuwa asilimia 9.8, kiashiria cha uzalishaji wa sekta ya huduma kiliongezeka kwa asilimia 18.2, mauzo ya bidhaa yaliyongezeka kwa asilimia 17.7, na uwekezaji uliongezeka kwa asilimia 19.9. Msemaji wa Idara Kuu ya Takwimu ya China Bw. Fu Linghui amesema, “Kwa mujibu wa takwimu za mwezi Aprili, uchumi umeendelea kufufuka kwa utulivu, na hali za ajira na mfumuko wa bei wimekuwa tulivu. Kwa ujumla mwelekeo mzuri wa ukuaji wa uchumi haujabadilika.”

Wachambuzi wanaona kutokana na kuhimizwa na zoezi la utoaji wa chanjo ya COVID-19, uchumi wa China utaendelea kufufuka katika robo ya pili, na mchango wa matumizi kwa ukuaji wa uchumi pia utazidi kuongezeka. Bw. Fu amesema, “Kwanza, kufuatia kukufuka kwa uchumi na ongezeko la ajira, vipato vya watu viliongezeka katika robo ya kwanza, na hali hii itasaidia kuongezeka kwa matumizi. Pili, China imefanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona, na imani ya wateja imeimarika. Tatu, kutokana na kufufuka kwa uchumi, watu wana matarajio kuhusu ukuaji wa uchumi, na wanapenda kuongeza matumizi. Hivyo mchango wa matumizi kwa maendeleo ya uchumi unatarajiwa kuongezeka zaidi.”

Bw. Fu amesema ingawa uchumi wa dunia bado unakabiliwa na changamoto kutokana na janga la COVID-19, kufufuka kwa uchumi wa China kuna matarajio mazuri. Amesema, “Kwanza, uchumi wa dunia unaendelea kufufuka, na utahimiza mahitaji ya nje kwa maendeleo ya uchumi wa China. Pili, kwa upande wa ndani ya China, mahitaji pia yanaendelea kuongezeka. Tatu, sera za kuunga mkono kampuni nchini China zitaendelea kufanya kazi.”