Israel yaendelea kuishambulia Gaza baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo “kudhamiria” kuendelea na mashambulizi
2021-05-20 20:04:00| CRI

 

 

Israel imeendelea kuishambulia Gaza baada ya Waziri Mkuu wa Israel Bw. Benjamin Netanyahu kupuuza mwito wa Rais Joe Biden wa Marekani kupunguza mvutano kati ya pande hizo mbili.

Maofisa wa afya wa Palestina wamesema mashambulizi yaliyofanyika jana usiku yamesababisha kifo cha Mpalestina mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa, huku msemaji wa jeshi la Israel akitoa taarifa kuwa ndege za Israel zimefanya mashambulizi kwenye nyumba za viongozi watano wa kundi la Hamas ili kuharibu maghala ya silaha na kuondoa miundo mbinu ya kijeshi kwenye nyumba hizo.

Jeshi la Israel leo limesema zaidi ya maroketi 4,000 yamerushwa kutoka Gaza dhidi ya Israel, 610 kati ya hayo yaliangukia ndani ya Gaza na asilimia 90 yalizuiwa na mfumo wa ulinzi dhidi ya maroketi wa Iron Dome.

Hadi sasa watu 12 wameuawa kwa upande wa Israel na wengine 227 wameuawa kwa upande wa Palestina.