Huduma za ustawi wa watoto nchini China kugeukia kwenye ulinzi wa watoto wadogo
2021-05-25 18:06:15| Cri

Wizara ya Mambo ya Kiraia imesema China imepanga kurekebisha huduma zake za ustawi wa watoto na kumaliza mchakato wa mageuzi hadi kufikia mwaka 2025 na kugeukia kwenye mfumo wa huduma za ulinzi wa watoto.

Wizara hiyo imebainisha kuwa huduma za ustawi wa watoto nchini China zitakuwa zikishughulikia kuwahifadhi na kuwasaidia watoto wadogo ambao watakuwa wakiangaliwa na mamlaka ya mambo ya kiraia, na kwamba kwa sasa vituo vingi havifanyi kazi kutokana na idadi ya mayatima kupungua kwa asilimia 66 kutoka takwimu za mwaka 2012 hadi za sasa ambazo ni 190,000.

Zhao Yong, afisa wa wizara hiyo amesema karibu asilimia 70 ya vituo vya kuhudumia watoto vya ngazi ya kaunti vina wakazi chini ya 10 akiongeza kwamba kuna vituo vya kuhudumia watoto 1,217 katika nchi nzima. Hata hivyo amesema mapungufu yaliyopo ni kwamba watoto wengi zaidi wenye ulemavu na magonjwa makubwa hawahudumiwi kitaalamu.