Ripoti yaonesha mmoja kati ya watu wanne anakabiliwa na ukosefu wa maji salama ya kunywa nyumbani
2021-07-02 10:59:07| CRI

Shirika la afya duniani WHO na Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF wametoa ripoti ya pamoja ikionesha kuwa karibu mmoja kati ya watu wanne anakabiliwa na ukosefu wa maji salama ya kunywa nyumbani.

Ripoti hiyo pia imesema COVID-19 imeonyesha haja ya kuhakikisha kila mmoja anapata maji safi ya kunawa mikono. Wakati maambukizi ya virusi hivyo yanaanza, karibu theluthi moja ya watu wote duniani hawakuwa na uwezo wa kunawa mikono kwa maji na sabuni.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa kutoka mwaka 2016 hadi 2020, idadi ya watu wenye maji salama nyumbani duniani imeongezeka kutoka asilimia 70 hadi 74, huku upatikanaji wa huduma za usafi ukiongezeka kutoka asilimia 47 hadi 57 na upatikanaji wa vifaa vya kunawa mikono kwa maji na sabuni umeongezeka kutoka asilimia 67 hadi 71.

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa ingawa maendeleo yamepatikana, lakini maendeleo hayo bado hayatoshi, na imeeleza kuwa eneo la Afrika kusini mwa Sahara lina kiwango kidogo zaidi cha maendeleo kote duniani.