Viongozi wa China, Ufaransa na Ujerumani wazungumza kwa njia ya mtandao
2021-07-06 08:22:45| cri

 

 

Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa njia ya mtandao.

Rais Xi amesema hivi sasa dunia bado inakabiliwa na hali ya wasiwasi kutokana na janga la COVID-19, na China na nchi za Ulaya zinapaswa kuongeza maoni ya pamoja na ushirikiano, ili kutoa mchango muhimu kwa juhudi za kukabiliana na changamoto ya kimataifa.

Viongozi hao pia wamebadilishana maoni kuhusu suala la Afrika, ambapo Rais Xi amesema China imetoa na inatoa chanjo ya COVID-19 kwa zaidi ya nchi 40 barani Afrika, na kufikia makubaliano ya kuchelewesha kulipa madeni na nchi 19 za Afrika. Amezikaribisha Ufaransa na Ujerumani kujiunga na Pendekezo la Wenzi wa Kuiunga Mkono Afrika Kupata Maendeleo lililotolewa na China pamoja na Afrika, na kufanya ushirikiano wa pande nyingi. 

Rais Macron ameipongeza China kwa kuzisaidia nchi zinazoendelea kupata chanjo ya COVID-19, na kusema nchi yake inapenda kuimarisha uratibu na China katika kuisaidia Afrika kupata mitaji na kuendeleza elimu.

Naye Bi. Merkel amesema Ujerumani inapenda kuongeza ushirikiano na China katika mambo ya kimataifa, haswa mabadiliko ya tabianchi, anuwai ya viumbe na kusaidia Afrika kukabiliana na janga la COVID-19, na pia itachunguza uwezekano wa kujiunga na Pendekezo la Wenzi wa Kuiunga Mkono Afrika Kupata Maendeleo.