Watu 12 wafa kwa mvua kubwa mjini Zhengzhou, China
2021-07-21 09:01:47| CRI

Jumla ya watu 12 wamekufa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha katika eneo la katikati la Zhengzhou, mji mkuu wa mkoa wa kati wa Henan nchini China.

Kwa mujibu wa serikali ya huko, watu wapatao laki moja wamehamishiwa kwenye maeneo salama.

Kiwango cha jumla cha mvua zilizonyesha Zhengzhou kilifikia wastani wa milimita 449 kuanzia saa 12 Jumapili hadi usiku wa manane jana Jumanne. Idara za hali ya hewa za mkoa wa Henan na mji wa Zhengzhou zote ziliinua kiwango cha mwitikio wa dharura kwa majanga ya hali ya hewa hadi kufikia ngazi ya kwanza.

Zaidi ya treni 160 zilisitisha huduma katika kituo cha treni cha Zhengzhou Mashariki, na kukwamisha idadi kubwa ya abiria.

Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua kubwa mkoani Henan zinatarajiwa kuendelea kunyesha hadi leo usiku.