Umoja wa Mataifa wataka juhudi zaidi zifanyike kutimiza malengo ya maendeleo endelevu kwa kubadili mfumo wa chakula
2021-07-27 08:47:36| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa juhudi zaidi za pamoja ili kutimiza Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kufanya mabadiliko katika mfumo wa sasa wa chakula.

Akizungumza katika mkutano wa utangulizi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mfumo wa Chakula utakaofanyika Septemba mwaka huu, Bw. Guterres amesema umasikini, ukosefu wa usawa wa kipato na gharama kubwa ya chakula vimeendelea kuwafanya watu bilioni 3 kushindwa kupata lishe bora. Pia amesema, mabadiliko ya tabianchi na vurugu vyote ni matokeo na vyanzo vya janga hili.

Guterres amesema, watu milioni 811 walikabiliwa na njaa mwaka jana kutokana na vikwazo vilivyosababishwa na janga la virusi vya Corona. amesisitiza kuwa, janga hilo ambalo bado linaendelea kuikumba dunia, limeweka wazi uhusiano kati ya dunia na ukosefu wa usawa, umasikini, chakula, na magonjwa.