Kundi la Taliban lateka miji mikuu ya majimbo matatu ndani ya siku moja
2021-08-09 09:09:21| cri

Msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid alisema tarehe 8 mwezi huu kupitia mtandao wa kijamii kwamba kundi hilo limeuteka Taloqan, mji mkuu wa jimbo la Takhar, ukiwa ni wa tatu kutekwa na kundi hilo siku hiyo. Mapema jana Jumapili Mujahid alitangaza kuwa Taliban limeteka miji mikuu ya majimbo ya Kunduz na Sar-e Pol.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan Fawaad Aman akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo alisema kikosi maalumu cha serikali kimekuwa kikifanya operesheni ya kuwasaka wapiganaji wa kundi la Taliban katika mji wa Kunduz lakini hakusema lolote kuhusu hali ya mapigano huko Sar-e Pol na Taloqan.

Jeshi la Marekani lilianza kuondoka Afghanistan tangu tarehe mosi Mei na Rais Biden alisema operesheni zote za kijeshi za Marekani zitaisha ifikapo tarehe 31 Agosti. Kufuata kuondoka huko, mapigano kati ya kundi la Taliban na jeshi la serikali ya Afghanistan yanaendelea vikali na kusababisha hali ya usalama kuwa mbaya.