Kampuni za Kenya zashirikiana kuinua mwamko wa kuwalinda Simba
2021-08-11 09:15:27| CRI

Kampuni ya Tusk kwa kushirikiana na kampuni ya Safaricom na Benki ya biashara ya Kenya KCB, wamezindua kampeni ya kuinua mwamko wa kuwalinda Simba barani Afrika.

Ikiwa ni sehemu ya kampeni hiyo, kampuni hizo zimetengeneza sanamu 47 za Simba zitakazowekwa kwenye mitaa mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na Nairobi, na katika baadhi ya miji nchini Uingereza, Marekani na Australia.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na makampuni hayo mjini Nairobi kwenye maadhimisho ya siku ya Simba duniani ambayo ilikuwa jana, imesema sanamu hizo zitawekwa ili watu wazifurahie hadi mwisho mwa mwezi Septemba.

Akiongea kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo waziri wa utalii na ulinzi wa wanyamapori wa Kenya Bw. Najib Balala, amesema Simba ni sehemu muhimu ya wanyama anuwai nchini Kenya na juhudi zinatakiwa kufanyika ili kuwalinda.