Mwanamke wa Tanzania auawa na tembo waliovamia makazi yao
2021-08-11 09:51:51| CRI

Polisi wa Tanzania wamesema mwanamke mwenye umri wa miaka 43 ameuawa na tembo waliovamia kijiji kimoja katika mkoa wa Kagera nchini humo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Bw. Revocatus Malimi, amesema tembo hao walimshambulia na kumuua mwanamke huyo juzi saa 4 usiku wakati anakwenda kuwatembelea majirani.

Wanakijiji walijaribu kupiga mayowe kuwafukuza tembo hao. Bado haijulikani kuna tembo wangapi, kwa sababu ajali hiyo ilitokea usiku.

Katika miaka ya hivi karibuni, ingawa serikali ya Tanzania imefanya juhudi kudhibiti wanyamapori, lakini matukio ya wanyama kuwaua wanakijiji na kuharibu mazao mashambani bado yanaongezeka.