Abiria saba kutoka Komoro wafa maji pwani ya kaskazini ya Kenya
2021-08-11 09:00:44| CRI

Abiria saba kutoka Komoro waliokuwa kwenye boti wamekufa maji umbali wa kilomita kadhaa kutoka pwani ya kaskazini ya Kenya.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne mjini Nairobi na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), inasema raia wengine wanane kutoka Komoro waliokolewa Jumatatu jioni baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kukumbwa na hitilafu ya injini na kupinduka kutokana na mawimbi makubwa katika bahari ya Hindi.

Manusura hao wakiwemo wanawake wawili, waliokolewa na wavuvi na Walinzi wa Pwani wa Kenya, na sasa wamepelekwa hospitali.