Kenya na Somalia zakubaliana kurejesha uhusiano uliokwama
2021-08-11 09:00:11| CRI

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya jana Jumanne alifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Somalia Bw. Mohamed Roble ambaye yuko ziarani nchini Kenya, ambapo wamekubaliana kurejesha uhusiano wa nchi hizo mbili uliokwama kwa miezi kadhaa.

Kwenye mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Mombasa, rais Kenyatta alisisitiza haja ya kuongeza ushirikiano kwenye masuala ya usalama, biashara na uwekezaji kupitia kutekeleza kikamilifu Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano ya 2015 (JCC) ili kupata ustawi.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikwama kwa miezi kadhaa baada ya serikali ya Somalia kuishutumu Kenya kukiuka mamlaka yake na kuingilia mambo yake ya kisiasa.

Kwa upande wake, Bw. Roble alijutia kuzorota kwa uhusiano wa Somalia na Kenya, akisema lilikuwa kosa kwa nchi hizo mbili kuachana na moyo wa mshikamano uliowekwa na baba waanzilishi wa nchi hizo mbili.