Watu 16 watekwa nyara baada ya shambulizi katika chuo kaskazini magharibi mwa Nigeria
2021-08-17 08:58:32| CRI

 

 

Watu 16 wametekwa nyara baada ya watu wasiojulikana waliokuwa na silaha kushambulia chuo kimoja kilichoko mkoani Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Msemaji wa jeshi la polisi mkoani Zamfara Mohammed Shehu amesema, Jumapili usiku, watu hao waliokuwa na silaha walivamia Chuo cha Kilimo na Sayansi ya Wanyama katika eneo la Bakura mkoani humo, na kuua polisi mmoja na walinzi wawili, na kuteka nyara wanafunzi 15 na wafanyakazi 4.

Shehu amesema, polisi wamewaokoa wafanyakazi watatu kwenye msitu ulio karibu, ambao watachunguzwa afya zao kabla ya kurudishwa kwenye familia zao. Amesema polisi na vikosi vingine vya usalama vinawasaka washambulizi hao, na kuwaokoa watu wengine waliotekwa nyara.