Mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini yasababisha vifo vya watu wasiopungua 27
2021-08-18 08:41:27| CRI

Watu wasiopungua 27 wameuawa na wengine 29 wamejeruhiwa katika siku mbili zilizopita kutokana na mapingano ya kikabila yaliyotokea katika jimbo la Warrap nchini Sudan Kusini.

Waziri wa Habari wa Jimbo la Warrap Bw. Riing Deng Ading amesema mapigano hayo yalianza Jumapili kati ya makabila ya Luany-Jang, Lou Paher na Thiik. Kwa sasa viongozi wa eneo hilo wanafanya juhudi kurudisha hali ya usalama katika maeneo yaliyoathiriwa.

Bw. Deng amewataka vijana kutoka makabila hasimu katika jimbo la Warrap kuacha mapigano na kufanya mazungumzo, ambayo ni njia pekee ya kuleta amani na utulivu katika jimbo hilo.

Tangu mwaka 2019, Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na mapigano ya kikabila katika majimbo ya Jonglei, Warrap na Lakes, hasa kutokana na wizi wa ng'ombe, utekaji nyara wa watoto na mauaji ya kulipiza kisasi.