Africa CDC yaunga mkono mifumo ya afya yenye ustahimilivu ili kuimarisha mwitikio wa janga la Corona
2021-08-19 11:16:25| Cri

Ofisa wa Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) amesema ni muhimu kuongeza ustahimilivu wa mifumo ya afya ya Afrika ili kuimarisha uwezo wa bara hilo wa kuhimili athari za janga la Covid-19.

Mshauri mwandamizi wa afya ya umma wa Africa CDC Ebere Okereke amesema hayo alipohojiwa na shirika la habari la China Xinhua kwa njia ya video jana Jumatano.

Amesema uwekezaji wa nyongeza unahitajika kuhuisha mifumo ya afya ya umma barani Afrika kupitia mafunzo, usimamizi wa magonjwa, manunuzi ya vifaa vya utambuzi wa magonjwa na dawa muhimu.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, ajenda 2063 ya Africa CDC imesisitiza haja kwa Afrika kujenga mfumo imara wa afya ya umma, ukiweka mkazo katika kuzuia maradhi na kuhimiza huduma bora za matibabu kama sharti la kutimiza mageuzi.