EAC yatoa wito kwa wawekezaji wa Kenya, Tanzania kuhimiza biashara ya kuvuka mpaka
2021-08-19 08:06:42| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa wito kwa wawekezaji wa Kenya na Tanzania kutumia fursa ya ushirikiano kati ya nchi hizo kuhimiza biashara ya kuvuka mpaka.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Peter Mathuki, amesema uagizaji wa bidhaa wa Kenya kutoka Tanzania kati ya mwezi Januari na Juni ulikua kwa asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho, kutokana na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya nchi hizo mbili yaliyolenga kutatua migongano ya kibiashara.

Takwimu za serikali ya Kenya zinaonyesha kuwa thamani ya bidhaa zilizoingizwa na kutoka Tanzania ilikuwa karibu dola za kimarekani milioni 167.5 katika nusu ya kwanza ya 2021, wakati thamani ya bidhaa zilizosafirishwa na Kenya kwenda Tanzania ikiwa ni dola za kimarekani milioni 158.

Bw. Mathuki amesema sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iko katika hatua za mwisho kuanzisha mfumo wa kufanya kazi wa saa 24 katika maeneo ya mpakani kwenye nchi zote wanachama, na kuunganisha kikamilifu mifumo ya vituo vya mpakani ili kuhimiza biashara.