Mafuriko katika mji mkuu wa Ethiopia yasababisha vifo vya watu saba
2021-08-19 08:06:07| CRI

Mafuriko yaliyotokea jana katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa yamesababisha vifo vya watu wasiopungua saba. Kamishna wa idara ya zimamoto na majanga ya Addis Ababa Bw. Solomon Fisseha, amesema mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha Jumanne pia yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Mwezi uliopita Kamisheni ya taifa ya kudhibiti maafa ya Ethiopia ilisema karibu watu milioni 2 wako kwenye hatari ya kukumbwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua unaoendelea. Kwa sasa Ethiopia iko katikati ya msimu wa mvua ambao ulianza mwezi Juni na unatarajiwa kuendelea hadi katikati ya Septemba.

Kwa sasa serikali ya Ethiopia inachukua hatua za tahadhari za majanga ya asili na kazi ya ukarabati katika maeneo yaliyoathiriwa.