Zambia yafanya sherehe ya kuapishwa kwa rais mpya
2021-08-25 09:58:27| CRI

Zambia jana ilifanya sherehe ya kuapishwa kwa rais mpya Hakainde Hichilema kwenye Uwanja wa michezo wa mashujaa mjini Lusaka.

Hichilema akihutubia sherehe hiyo amesema serikali yake itafanya juhudi kwa ajili ya maslahi ya wananchi wake wote. Serikali mpya itarekebisha na kukuza uchumi, ili kuwawezesha watu waondokane na umaskini. Serikali itatekeleza ahadi zilizotolewa kwenye kampeni za uchaguzi, na kurejesha utawala wa kisheria na heshima ya wananchi.

Amemshukuru rais wa zamani kwa kutoa mchango kwa ajili ya nchi hiyo pamoja na kufanikiwa kukabidhiana madaraka ya uongozi kwa amani. Pia amekaribisha sekta binafsi zishirikiane na serikali katika kukuza uchumi, na kukaribisha vyama mbalimbali vya kisiasa vishirikiane na chama tawala kwa kusitisha mpasuko wa kisiasa.

Habari zaidi zinasema rais Xi Jinping wa China amemtumia salamu Hakainde Hichilema, na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Zambia. Kwenye salamu zake rais Xi amesema China na Zambia ni marafiki, wenzi na ndugu wakubwa, na tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi zimeimarisha hali ya kuaminiana katika mambo ya kisiasa, na ushirikiano katika sekta mbalimbali, zaidi ya hayo zimeelewana na kuungana mkono katika masuala muhimu yanayohusisha maslahi yao makuu na zinayoyafuatilia kwa pamoja. Ameeleza kuwa anatilia maanani sana maendeleo ya uhusiano kati ya China na Zambia, na kuthamini urafiki wa jadi kati ya nchi zao. Pia ameongeza kuwa anapenda kushirikiana na rais Hichilema katika kukuza ushirikiano, ili kuzinufaisha nchi hizo mbili na wananchi wao.