China na Afrika kutekeleza “Mpango wa wenzi wa uvumbuzi wa kidijitali”
2021-08-26 10:41:20| CRI

China na Afrika kutekeleza “Mpango wa wenzi wa uvumbuzi wa kidigitali”_fororder_1

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin amesema ubunifu wa kidijitali ni sekta iliyojitokeza hivi karibuni kwa ushirikiano wa kivitendo kati ya China na Afrika, na China inapenda kushirikiana na Afrika katika kutunga na kutekeleza “Mpango wa wenzi wa uvumbuzi wa kidijitali kati ya China na Afrika”.

Msemaji Wang ameeleza kuwa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi alipokuwa kwenye ziara yake barani Afrika mwanzoni mwa mwaka huu alisema, China itaimarisha ushirikiano wa kidijitali na Afrika na kuisaidia kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na mapinduzi ya TEHAMA, kuondoa pengo la kidijitali na kuijenga Afrika kuwa ya kidigitali.

Msemaji huyo ameongeza kuwa vitendo ni muhimu kuliko maneno, na wakati China inapotangaza mpango huo wa wenzi, ahadi husika zimeanza kubadilika kuwa hali halisi. Miradi mikubwa ya mtandao wa mkonga wa mawasiliano chini ya ushirikiano kati ya China na Afrika itaanza hivi karibuni barani Afrika, kuanzia mwezi Septemba kutakuwa na msimu wa kukuza biashara ya mtandaoni kwa bidhaa za Afrika, Kongamano la Ushirikiano wa Beidou kati ya China na Afrika na shughuli nyingine. China itadumisha mawasiliano na Afrika ili kutunga kwa pamoja hatua za ushirikiano wa kivitendo katika sekta ya dijitali kwa ajili ya miaka mitatu ijayo na kuzijumuisha kwenye makubaliano ya mkutano wa FOCAC utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu ili kuinua ushirikiano wa kidijitali kati ya pande hizo mbili kwenye ngazi mpya.