Waziri wa Mambo ya Nje wa China asema China itaimarisha ushirikiano wake na Ethiopia na Afrika kwa ujumla
2021-08-26 10:35:16| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema China iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kivitendo na Ethiopia katika maeneo mbalimbali na kutumia fursa ya mkutano ujao wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kutoa msukumo mpya kwenye ushirikiano wa pande hizi mbili.

Kwenye mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ethiopia ambaye pia ni naibu waziri mkuu, Demeke Mekonnen, Wang amesema China na Ethiopia ni wenzi wakubwa wa ushirikiano wa kimkakati na kwamba uhusiano wao umepitia majaribu mengi na kuwa imara baada ya muda. Kuhusu janga la UVIKO-19, Bw. Wang amesema nchi hizo mbili zimesaidiana, na China iko tayari kuendeleza uratibu na ushirikiano wa karibu na Ethiopia katika masuala ya kimataifa na kulinda maslahi ya pamoja ya pande hizi mbili pamoja na nchi nyingine zinazoendelea.

Naye Bw. Demeke ameishukuru China kwa kuiunga mkono Ethiopia katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona akisema nchi yake imedhamiria kuupandisha ushirikiano wa kina wa wenzi wa kimkakati katika ngazi ya juu.