Askari 13 wa Marekani na raia 60 wa Afghanistan wauawa kwenye shambulizi lililofanywa na IS mjini Kabul
2021-08-27 10:02:38| CRI

Askari 13 wa Marekani na raia 60 wa Afghanistan wauawa kwenye shambulizi lililofanywa na IS mjini Kabul_fororder_1

Ijumaa Afghanistan ilishuhudia mlipuko mwingine mkubwa katika mji mkuu wake Kabul, baada ya milipuko ya mabomu mawili kusababisha vifo vya watu kadhaa, wakiwemo askari wa jeshi la Marekani kwenye Uwanja wa Ndege wa Kabul.

Hata hivyo msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amefafanua kwenye taaarifa yake kupitia twitter kwamba lilikuwa ni bomu lililodhibitiwa na wanajeshi wa Marekani ili kuharibu vifaa vya uwanja wa ndege. Kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani Kenneth McKenzie alithibitisha kuwa wanajeshi wake 12 waliuawa na wengine 15 kujeruhiwa kwenye shambulizi hilo.

Mashambulizi hayo ni makubwa sana nchini Afghanistan dhidi ya askari wa Marekani, ambapo McKenzie amesema shambulizi moja lilitokea kwenye lango la Abbey la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai, na jingine karibu na Hoteli ya Baron. Lile la lango la Abbey ambalo limesababisha wahanga wengi wa Marekani, limefanywa na mtu aliyejitoa muhanga na kufuatiwa na watu kadhaa wenye silaha wa kundi la IS ambao waliwafyatulia risasi raia na vikosi vya jeshi, na matokeo yake hata raia wa Afghanistan pia wameathirika.

Awali kundi la IS lilidai kuhusika na shambulizi hilo, likisema liliwalenga watafsiri na washirika wa jeshi la Marekani. Kwenye taarifa yao kundi hilo lilibainisha kuwa mtu aliyejitoa muhanga alifanikiwa kuingia kwenye mkusanyiko mkubwa wa watafsiri na washirika wa jeshi la Marekani kwenye kambi ya Baran karibu na Uwanja wa Ndege wa Kabul, na kulipua mkanda wake wa bomu, ambapo alisababisha vifo vya watu 60 na kujeruhi zaidi ya 100. Lakini kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Afghanistan, watu waliouawa ni 73 wakiwemo 13 wa Marekani na 60 wa Afghanistan huku 155 wakijeruhiwa.

Kamanda McKenzie alipokuwa kwenye mkutano na Wizara ya ulinzi alisema vikosi vya Marekani vilivyopo Afghanistan vinakabiliwa na vitisho vikubwa kutoka makundi ya kigaidi, hasa ISIS-K, ambalo lina uhusiano na IS na ambalo Taliban linapambana nalo.

Naye Mwenyekiti wa Mkutano wa 75 wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) Volkan Bozkir jana Alhamis alitoa wito wa kuwalinda raia na kuwapatia haki yao ya uhuru, hasa akisistiza wanawake na watoto lazima wapewe kipaumbele. Amesema kwa miaka 40 Baraza Kuu limekuwa likishughulikia hali nchini Afghanistan, likilenga amani, utulivu, utawala bora, haki za binadamu na maendeleo.

Kwa upande wake waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Uingereza itaendelea na zoezi lake kuwahamisha watu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kabul hadi mwisho licha ya mashambulizi hayo ya mabomu. Amesisitiza kuwa tishio hilo la ugaidi ni moja ya vizuizi ambavyo wamekuwa wakishughulikia, na wamejiandaa navyo.