Pembe ya Afrika kukabiliwa na uhaba wa mvua
2021-08-27 10:00:11| CRI

Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) jana lilikadiria kuwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba, eneo la pembe ya Afrika litakabiliwa na uhaba wa mvua, na kufanya hali iwe mbaya zaidi ya usalama wa chakula na maji kwenye eneo hilo.

IGAD imekadiria kuwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu, Afrika Mashariki itakabiliwa na msimu wenye ukame zaidi, hali ambayo itasababisha uhaba wa mvua na kupunguza mavuno ya mazao, pamoja na kuongeza idadi ya watu watakaokumbwa na balaa la njaa. Inakadiriwa kuwa Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya, Somalia, Ethiopia na Eritrea zitakumbwa na ukame, ambao utavuruga shughuli za kulima kwenye kipindi hicho cha mwezi Oktoba hadi Disemba.

IGAD imeongeza kuwa hali ya ukame kwenye maeneo ya mpaka kati ya Kenya na Somalia imekuwa mbaya zaidi, na halijoto itaikumba pembe ya Afrika, hali ambayo italeta balaa la njaa na utapiamlo mkali na kuweza kusababisha msukosuko wa kibinadamu kwenye eneo hilo.