Pande hasimu za Sudan Kusini zafikia makubaliano ya kuwa makao makuu ya pamoja ya jeshi
2021-08-30 08:43:07| CRI

Pande hasimu za Sudan Kusini zimefikia makubaliano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu ya kuundwa kwa kituo kimoja cha uongozi wa jeshi, kabla watumishi elfu 83 wa kikosi kilichounganishwa hawajahitimu mafunzo yao.

Waziri wa maswala ya baraza la mawaziri Bw Martin Elia Lomuro, amesema makubaliano hayo yaliyofikiwa yanakomesha hali ya kukwama kuhusu mgao wa nafasi ndani ya jeshi. Amesema kwa sasa kundi la SPLM upande wa serikali litachukua asilimia 60 ya nafasi za jeshi, na kundi la SPLM upande wa upinzani litachukua asilimia 40 ya nafasi hizo.

Rais Salva Kiir na makamu wake Bw. Riek Machar wanaongoza makundi hayo hasimu, wamekuwa na tofauti kuhusu mgao wa nafasi hizo.

Watumishi wanaotarajiwa kuhitimu na kujiunga na kikosi cha pamoja ni polisi, wanajeshi, idara ya ujasusi na walinzi wa wanyamapori, watakaochukua nyadhifa zao kwenye kipindi cha mpito.