Sudan na Chad zasisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano ili kupambana na ugaidi na kulinda mpaka kati yao
2021-08-30 08:44:34| CRI

Sudan na Chad zimesisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano kati yao ili kupambana na changamoto za pamoja za ugaidi na msimamo mkali na kulinda mpaka wa pamoja.

Pande hizo mbili zimefanya mazungumzo kwenye ikulu ya Sudan, yakiendeshwa na mwenyekiti wa baraza tawala la Sudan Bw. Abdel-Fattah Al-Burhan na Rais wa baraza la mpito la kijeshi la Chad Bw. Mahamat Idriss Deby Itno.

Bw. Al- Burhan amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kwenye kupambana na changamoto za magaidi na makundi yenye msimamo mkali, na kutoa mwito wa kufufua makubaliano ya kulinda mpaka yaliyosainiwa mwaka 2018 mjini N'djamena na Sudan, Chad, Libya na Niger.

Bw. Mahamat Idriss Deby Itno amesema wana uwezo na nia ya kisiasa kupambana na maswala na changamoto zinazozikabili nchi hizo mbili. Amesema licha ya kuwa nchi yake iko kwenye kipindi cha mpito, wanatarajia uungaji mkono kutoka Sudan ikiwa ni nchi jirani na rafiki.