Uganda yawaokoa wanawake 8 wa Burundi kutoka kwa wafanyabiashara wa magendo ya binadamu
2021-09-01 10:06:11| CRI

Uganda imewaokoa wanawake 8 wa Burundi kutoka kwa watuhumiwa wa magendo ya binadamu.

Naibu mratibu wa taifa wa kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu katika kamati ya udhibiti wa uraia na uhamiaji Bibi Agnes Igoye amesema, wanawake hao wenye umri kutoka 18 hadi 30 walikuwa wanasafirishwa kuelekea nchi nyingine isiyofahamika.

Bibi Igoye amesema wanawake hao waliletwa nchini Uganda na kupelekwa Kenya na baadaye kurudishwa Uganda. Wafanyabiashara wa magendo ya binadamu walijaribu kuwachanganya wana usalama kabla ya wanawake hao kusafirishwa kwenda nchi nyingine.

Ofisa huyo pia amesema Uganda inatumiwa kama mapito kwa wafanyabiashara ya magendo ya binadamu ambao wanachukua wasichana na wanawake kutoka Burundi, na kuwaahidi kuwapeleka kufanya kazi Mashariki ya Kati.