Wataalam wasema chanjo ya COVID-19 itaamua maendeleo ya Afrika
2021-09-01 09:00:09| CRI

Maofisa na wataalam wa Afrika wameonesha mashaka kuhusu maendeleo ya uchumi wa nchi za Afrika kutokana na kuwa asilimia kubwa ya watu barani Afrika bado wanaendelea kutokuwa na chanjo.

Taarifa iliyotolewa kwenye kamati ya uchumi wa Afrika ya Umoja wa mataifa imesema kwenye mkutano kuhusu kufufuka kwa uchumi wa Afrika, maofisa na wataalamu hao wameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya utoaji wa chanjo barani Afrika.

Akiendesha mkutano huo katibu mtendaji wa kamati ya uchumi wa Afrika ya Umoja wa mataifa Bibi Vera Songwe, amesema maendeleo ya uchumi wa Afrika yatatokana na utoaji wa chanjo ya COVID-19.

Hadi sasa ni asilimia 2.3 tu ya watu bilioni 1.3 barani Afrika ndio wamepata chanjo. Ili kupata kinga ya jamii asilimia 60 hadi 70 ya watu wote wanatakiwa kupata chanjo, lakini hadi sasa Afrika imepata chanjo milioni 400, lakini inahitaji chanjo bilioni 1.6.