EABC yatoa wito wa jeshi kufanya doria ili kuongeza usalama wa kibiashara
2021-09-07 08:48:07| CRI

Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limeitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuunda na kupeleka kikosi cha pamoja cha jeshi ili kusindikiza na kuwalinda madereva wa malori, wakati biashara ya kuvuka mpaka imesitishwa kutokana na hofu ya usalama.

Katika taarifa yake, Baraza hilo limesema, kupelekwa kwa jeshi hilo la usindikizaji litasaidia kuwezesha usafirishaji wa bidhaa muhimu wakati huu wa janga la COVID-19.

Taarifa hiyo imesema, kutokana na wasiwasi wa kiusalama nchini Sudan Kusini, hususan katika barabara ya mpakani ya Nimule-Elegu kuelekea Juba, zaidi ya malori 1,056 yamekwama mpakani, na kuhatarisha kuenea kwa virusi vya Corona katika jamii za mpakani.