China yafurahia Taliban kutangaza kuunda serikali ya muda
2021-09-09 11:51:59| cri

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Wang Wenbin jana alisema China inatilia maanani juu ya Taliban kutangaza kuunda serikali ya muda nchini Afghanistan pamoja na mambo muhimu kadhaa kuhusu upangaji wa watu.

Amesema hatua hiyo inamaliza mvurugano wa zaidi ya wiki tatu wa nchi kutokuwa na serikali, hatua ambayo ni mchakato wa lazima katika kurejesha utaratibu na kujenga upya nchi baada ya vita. Aidha amesema msimamo wa China juu ya suala la Afghanistan ni thabiti, ambao ni kushikilia sera ya kutoingilia mambo ya ndani, na kwamba inaheshimu uhuru wa mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa Afghanistan, na kuwaunga mkono watu wa Afghanistan wachague njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi ya nchi. Habari zinasema Taliban ilitangaza kuunda serikali ya muda Jumanne wiki hii, ambapo Mullah Hassan Akhund ameteuliwa kuwa kaimu waziri mkuu.