Wataalam wasema mfumo nyumbufu wa chakula wa China waivutia Afrika wakati wa janga la COVID-19
2021-09-09 08:54:24| CRI

Wataalamu wa Afrika na China wamesema, uwezo wa China wa kudumisha unyumbufu wa mfumo wake wa kilimo na chakula wakati wa janga la virusi vya Corona umekuwa mfano wa kuigwa na nchi za bara hilo.

Wakizungumza kando ya mkutano wa kilele wa Jukwaa la Mageuzi ya Kijani Afrika (AGRF) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya, kwa njia ya mtandao, wataalamu hao wamesema Afrika inapaswa kuiga mambo mazuri kutoka China ikiwemo matumizi ya biashara kupitia mtandao wa internet ili kupunguza athari za janga la virusi vya Corona katika mnyororo wa thamani ya bidhaa za kilimo.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema, nchi za Afrika ziko tayari kujifunza mafanikio ya China katika kukwepa vizuizi katika mfumo wake wa chakula wakati wa janga hilo.

Mkurugenzi mtendaji na mtafiti kutoka Taasisi ya Habari za Kilimo iliyo chini ya Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya China, Nie Fengyin amesema, kuongezeka kwa matumizi ya biashara kwa njia ya kielektroniki kumeonyesha mafanikio katika kudumisha mnyororo wa usambazaji wa chakula, hata wakati hatua kali za kudhibiti virusi vya Corona zilipokuwa zinatekelezwa.